Magaidi sita waangamizwa na maafisa usalama kusini mwa Misri
(last modified Sun, 13 Jan 2019 07:50:57 GMT )
Jan 13, 2019 07:50 UTC
  • Magaidi sita waangamizwa na maafisa usalama kusini mwa Misri

Wanachama sita wa genge moja la kigaidi wameuawa katika operesheni ya maafisa usalama huko kusini mwa Misri.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, magaidi hao wakufurishaji waliuawa katika operesheni ya jana Jumamosi katika mkoa wa Sohag, yapata kilomita 460 kusini mwa mji mkuu Cairo.

Taarifa ya wizara hiyo imeongeza kuwa, silaha kadhaa zikiwemo bunduki, risasi na mada za miripuko zimepatikana katika maficho ya magaidi hao wa kitakfiri.

Operesheni hiyo inaonekana kuwa ya ulipizaji kisasi haswa kwa kuzingatia kuwa, imefanyika siku chache baada ya wanajeshi watano wa Misri kuuawa katika shambulizi la bomu katika mji wa al Arish katika mkoa wa Sinai Kaskazini.

Magaidi wakufurishaji katika Rasi ya Sinai

Ukosefu wa amani na mashambulizi ya kigaidi yamekuwa yakishuhudiwa kila uchao nchini Misri katika miaka ya karibuni, hususan baada ya kupinduliwa serikali ya Muhammad Morsi, rais halali wa Misri aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia.

Rais huyo wa Misri alipinduliwa mwaka 2013 katika mapinduzi yaliyoongozwa na Abdul Fattah al Sisi, Rais wa sasa wa Misri. 

Tags