Mwito wa SADC wa kuhesabiwa upya kura DRC wapokewa kwa hisia tofauti
Mwito uliotolewa jana na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC wa kutaka kuhesabiwa upya kura na kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umepokewa kwa hisia tofauti huku baadhi wakionesha kushangazwa na mwito huo na wengine wakiupokea kwa tahadhari kubwa. Mwito huo wa SADC umekuja kutokana na kuendelea mzozo kuhusu matokeo ya uchaguzi wa rais wa Desemba 30, 2018 huko DRC.
Ukitoa hisia zake kuhusu mwito huo, muungano wa vyama tawala unaoongozwa na Rais Joseph Kabila (FCC), umesema umepokea taarifa hiyo kwa tahadhari kubwa na hauna uhakika na usahihi wake. Kodjo Ndukuma, mmoja wa wasemaji wa FCC, alisema hayo jana usiku baada ya kutolewa waraka wa mwito huo uliosainiwa na mshauri wa rais wa Zambia anayehusika na masuala ya uhusiano badala ya Namibia, ambayo ndiye mwenyekiti wa hivi sasa wa SADC.
Msemaji huyo wa FCC amesema, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wajibu wa kutatua mgogoro wa uchaguzi ni wa Mahakama ya Katiba.
Kwa upande wa muungano wa upinzani Lamuka umefurahishwa na mwito huo kiasi kwamba, mgombea Martin Fayulu anayedai kushinda katika uchaguzi huo amesema katika ujumbe wa Twitter kwamba, "amekaribisha" mwito huo wa SADC. Amesema: "Tunachotaka tu ni ukweli wa uchaguzi."
Kwa upande wake, muungano mwingine wa upinzani CASH wa Felix Tshisekedi umejizuia kutoa maoni yoyote kuhusu mwito huo wa SADC. Itakumbukuwa kuwa Tshisekedi anakwepa kuzungumza chochote tangu tume ya uchaguzi Ceni ilipomtangaza mshindi wa uchaguzi huo.