Misri yawaonya wanaopinga Saudia kupewa visiwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i5086-misri_yawaonya_wanaopinga_saudia_kupewa_visiwa
Serikali ya Misri imesema itawachukulia hatua wanaopanga kushiriki katika maandamano ya leo Ijumaa kupinga hatua ya rais wa nchi hiyo kuipa Saudia visiwa viwili muhimu katika Bahari ya Sham.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 15, 2016 03:38 UTC
  • Misri yawaonya wanaopinga Saudia kupewa visiwa

Serikali ya Misri imesema itawachukulia hatua wanaopanga kushiriki katika maandamano ya leo Ijumaa kupinga hatua ya rais wa nchi hiyo kuipa Saudia visiwa viwili muhimu katika Bahari ya Sham.

Katika taarifa, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri imesema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watu watakaoitikia mwito huo kwa kujitokeza leo na kuandamana kupinga uamuzi huo wa Rais Abdel Fattah el Sisi.

Muungano wa kitaifa unaounga mkono serikali ya kidemokrasia na kupinga mapinduzi ya jeshi nchini Misri umetaka yafanyike maandamano kote nchini humo kulalamikia hatua ya Rais wa nchi hiyo ya kuipatia Saudi Arabia visiwa viwili vya nchi hiyo.

Muungano huo umeongeza kuwa, wananchi wa Misri kamwe hawatafumbia macho mamlaka ya kujitawala ya visiwa viwili vya Sanafir na Tiran.

Wakati wa safari ya Mfalme Salman wa Saudi Arabia nchini Misri siku chache zilizopita, serikali ya Misri ilitangaza rasmi kutiwa saini makubaliano ya mipaka ya baharini kati ya nchi hiyo na Saudi Arabia; na kwa mujibu wa makubaliano hayo, Misri imeipatia Saudia visiwa viwili vya Sanafir na Tiran. Tangazo hilo la kushtukiza limeamsha hasira na malalamiko ya Wamisri ambao walikuwa wakivitambua visiwa hivyo kuwa ni ardhi yao kwa miongo mingi.

Wananchi wa Misri wameikosoa na kuipinga vikali serikali kwa hatua yake ya kusaini makubaliano hayo na serikali ya Riyadh.

Wanaharakati mbalimbali nchini Misri wametoa maoni yao wakisema kuwa Rais al Sisi anauza ardhi ya Misri kwa muitifaki tajiri kupitia mapatano ya udhalilishaji.