Maandamano Zimbabwe baada ya ongezeko la bei ya mafuta kwa 150%
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50867-maandamano_zimbabwe_baada_ya_ongezeko_la_bei_ya_mafuta_kwa_150
Wananchi wa Zimbabwe hii leo wamefanya maandamano katika miji mikubwa ya nchi hiyo ukiwemo mji mkuu Harare, kulalamikia ongezeko la bei ya fueli kwa asilimia 150 lililotangazwa jana na Rais Emmerson Mnangagwa wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 14, 2019 15:30 UTC
  • Maandamano Zimbabwe baada ya ongezeko la bei ya mafuta kwa 150%

Wananchi wa Zimbabwe hii leo wamefanya maandamano katika miji mikubwa ya nchi hiyo ukiwemo mji mkuu Harare, kulalamikia ongezeko la bei ya fueli kwa asilimia 150 lililotangazwa jana na Rais Emmerson Mnangagwa wa nchi hiyo.

Waandamanaji hao wamefunga barabara kuu za miji hiyo katika maandamano hayo, huku baadhi ya waandamanaji wakifanya uharibifu mkubwa na wengine wakivunja maduka.

Maafisa wa polisi wametumia mabomu ya kutoa machozi kukabaliana na waandamanaji katika mji wa kusini wa Bulawayo, ambao wameteketeza kwa moto matairi huku wakiwazuia abiria kupanda mabasi ya uchukuzi wa umma.

Mmoja wa waandamanaji hao kwa jina Glen Ncube mwenye umri wa miaka 25 amenukuliwa na vyombo vya habari akisema, "Huyu ni mtu wa aina gani. Mnangagwa hapaswi hata kuitwa rais. Anafanya maisha kuwa magumu na anatumia polisi kutukandamiza tusipaze sauti zetu."

Walimu wakifanya maandamano mjini Harare

Haya yanajiri katika hali ambayo, watumishi wa umma nchini Zimbabwe kupitia miungano na vyama vya kutetea maslahi yao, Alkhamisi iliyopita walikataa nyongeza ya asilimia 10 ya mshahara iliyotangazwa na serikali.

 Walimu na madaktari nchini humo wamekuwa wakifanya mgomo wakisisitiza kuwa wanataka kulipwa mishahara yao kwa kutumia sarafu ya dola ya Marekani.

Rais Emmerson Mnangagwa