SADC yaitisha kikao cha dharura kujadili mgogoro wa kisiasa Kongo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50901-sadc_yaitisha_kikao_cha_dharura_kujadili_mgogoro_wa_kisiasa_kongo_dr
Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) inatazamiwa kufanya kikao cha dharura kesho Alkhamisi, kujadili mgogoro wa kisiasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, uliobuka baada ya kutangazwa matokeo tata ya uchaguzi wa urais.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 16, 2019 00:59 UTC
  • SADC yaitisha kikao cha dharura kujadili mgogoro wa kisiasa Kongo DR

Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) inatazamiwa kufanya kikao cha dharura kesho Alkhamisi, kujadili mgogoro wa kisiasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, uliobuka baada ya kutangazwa matokeo tata ya uchaguzi wa urais.

Mshauri wa masuala ya kidiplomasia wa rais anayeondoka mamlakani, Joseph Kabila ameliambia shirika la habaria la Reuters kuwa, mkutano huo wa dharura utafanyika katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa. Hata hivyo hakutoa maelezo ya kina juu ya mkutano huo wa viongozi wa kieneo.

Awali SADC ilisema DRC inapaswa kufikiria suala la kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa baada ya nchi hiyo kukumbwa na mivutano kufuatia kutangazwa matokeo tata ya uchaguzi wa urais uliofanyika Disemba 31 mwaka uliomalizika.

Martin Fayulu (kushoto) na Felix Tshesekedi

Hapo jana Jumatano  Mahakama ya Katiba ilianza kusikiliza kesi ya Martin Fayulu, mgombea wa upinzani ambaye anapinga matokeo ya uchaguzi huo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi, akisisitiza kuwa, yeye ndiye aliyeshinda uchaguzi huo kwa zaidi ya asilimia 60 ya kura, lakini Tume ya Uchaguzi ikamtangaza mshindani wake, Felix Tshisekedi kuwa mshindi.

Alkhamisi iliyopita, Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (CENI) ilimtangaza Felix Tshisekedi wa chama cha upinzani cha UDPS kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais, kwa kujipatia asilimia 38.57 ya kura, akiwatangulia wagombea Martin Fayulu wa Lamuka na Emmanuel Ramazani Shadary aliyewakilisha muungano wa chama tawala nchini humo.