Mahakama ya DRC yathibitisha kuwa Tshisekedi ndiye mshindi halali wa urais
Mahakama ya Katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imemtangaza Felix Tshisekedi kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais uliofanyika Disemba 30 mwaka uliomalizika.
Jaji Noel Kilomba wa mahakama hiyo amesema leo Jumapili kuwa, mgombea wa muungano wa upinzani wa Lamuka, Martin Fayulu ameshindwa kutoa ushahidi wa kuonesha kuwa matokeo ya uchaguzi huo yalikuwa na kasoro au yalichakachuliwa, na kwa msingi huo Tshisekedi ndiye mshindi halali wa uchaguzi huo. Amesema Tume ya Uchaguzi nchini humo CENI ndiyo imeweza kuithibitishia mahakama hiyo kuwa matokeo yake yalikuwa halali na ya kweli. Januari 10 CENI ilitangaza matokeo ya muda, yaliyoonesha kuwa Felix Tshisekedi ndiye mshindi wa kiti cha urais kwa kujinyakulia asilimia 38.57 ya kura huku Fayulu aliyeenda mahakamani kupinga matokeo hayo akiibuka wa pili kwa asilimia 34.8 ya kura.
Alkhamisi iliyopita, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilikataa wito wa Umoja wa Afrika (AU) wa kuchelewesha kutangaza matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa rais, kwa sababu ya "shaka kubwa" kuhusu jinsi uchaguzi huo ulivyofanyika. Mgombea wa muungano wa upinzani wa Lamuka, Martin Fayulu anasisitiza kwamba matokeo ya uchaguzi huo yamechakachuliwa kwa faida ya Felix Tshisekedi aliyetangazwa kuwa mshindi wa kiti cha rais, na kwamba ndiye aliyeshinda uchaguzi huo kwa kupata zaidi ya asilimia 60 ya kura. Ameitaka jamii ya kimataifa ikiwemo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kutokubali matokeo hayo, akisisitiza kuwa kumefanyika mapinduzi ya kikatiba nchini humo.