Hafla ya kumuapisha rais mpya wa Kongo DR yaakhirishwa
Sherehe za kumuapisha rais mpya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zilizotazamiwa kufanyika leo Jumanne zimeakhirishwa na sasa zitafanyika baadaye wiki hii.
Msemaji wa serikali ya DRC, Lambert Mende ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa, hafla hiyo ya kumuapisha rais mteule, Felix Tshisekedi haitafanyika leo, na yumkini itafanyika Alkhamisi ijayo.
Hata hivyo hajatoa maelezo na sababu za kuakhirishwa shughuli hiyo muhimu. Lakini muungano wa CASH ulioshinda uchaguzi huo unasema tukio hilo la kihistoria, limeakhirishwa ili kukamilisha maandalizi ya kupokezana madaraka kwa amani katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati.
Jana Jumatatu maafisa usalama nchini humo walisimamisha mkutano wa kisiasa wa muungano wa upinzani wa Lamuka. Polisi walivuruga mkusanyiko wa wafuasi wa aliyekuwa mgombea wa muungano huo, Martin Fayulu, waliokuwa wamekusanyika nje ya makao makuu ya chama hicho mjini Kinshasa.
Msemaji wa Fayulu, Eve Bazaiba amesema, "Polisi walivamia makao makuu ya chama chetu na kufunga malango ya kuingia na kutoka, huku wakiwatawanya wanachama wetu waliokuwa wamekusanyika hapo."
Fayulu hapo jana aliwataka viongozi wa Afrika kusikiliza sauti ya Wakongomani, waliyopaza kupitia kura.
Binafsi anasisitiza kuwa ndiye aliyeshinda uchaguzi wa rais wa Disemba 30 mwaka uliopita, kwa kupata zaidi ya asilimia 60 ya kura; msimamo unaoungwa mkono na Kanisa Katoliki nchini humo, lililokuwa na waangalizi wa uchaguzi wapatao 40 elfu katika maeneo yote ya nchi.
Mahakama ya Katiba nchini humo Jumapili iliyopita ilitupilia mbali kesi ya Fayulu ya kupinga matokeo ya Tume ya Uchaguzi CENI, yaliyomtangaza Tshisekedi kuwa mshindi wa uchaguzi huo kwa kuzoa asilimia 38 ya kura, huku ikitangaza kuwa Fayulu alipata asilimia 34.