Wanafunzi wanne wauawa katika ghasia Kongo
Wanafunzi watatu na afisa wa polisi wameaga dunia kufuatia ghasia zilizotokea kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya kukatika huduma ya umeme na maji.
Ghasia hizo ziliibuka jana baada ya eneo kubwa kikiwemo Chuo Kikuu cha Lubumbashi kukatiwa huduma ya umeme na maji kwa siku tatu mfululizo kwa sababu ya matatizo yaliyojitokeza katika kebo na mabomba ya maji. Matatizo hayo yalisababishwa na mvua nyingi zilizonyesha.
Mbali na kulalamikia kukatwa kwa umeme na maji, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Lubumbashi walikuwa wakilalamikia pia kupandishwa ada ya chuo.
Ghasia na vurumai zilishika kasi jana Jumapili baada ya polisi kutumia gesi ya kutoa machozi na kufyatua risasi angani ili kuwatawanya wanafunzi waliokuwa wakirejea kutoka katika makazi ya gavana wa mji huo huko Katanga ya Juu.
Taarifa kutoka ofisi ya Rais imeeleza kuwa afisa polisi aliyeamuru kupigwa risasi wanafunzi waliokuwa wakiandamana kwa amani kabla ya kuwatahadharisha kuwa atafikishwa katika mahakama ya kijeshi kujibu mashtaka. Aidha taarifa hiyo imeongeza kuwa nyongeza hiyo ya ada ya chuo iliyotangazwa imesitishwa.
Baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Lubumbashi wamenukuliwa wakisema kuwa tayari huduma ya maji na umeme imerejea chuoni hapo.