Watu wawili wafariki katika hujuma ya kigaidi Mogadishu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51198-watu_wawili_wafariki_katika_hujuma_ya_kigaidi_mogadishu
Watu wasiopungua wawili wamefariki dunia baada ya gari lililotegwa bomu kulipuka katika kituo cha mafuta karibu na makao makuu ya ofisi za kanda ya Banadir, mjini Mogadishu, Somalia, mapema leo Jumanne.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 29, 2019 10:28 UTC
  • Watu wawili wafariki katika hujuma ya kigaidi Mogadishu

Watu wasiopungua wawili wamefariki dunia baada ya gari lililotegwa bomu kulipuka katika kituo cha mafuta karibu na makao makuu ya ofisi za kanda ya Banadir, mjini Mogadishu, Somalia, mapema leo Jumanne.

Naibu Meya wa Mogadishu  Mohammad Tuulah amesema mlipuko huo umetokea wakati gari lililokuwa limesheheni mabomu lilipolipuka katika kituo cha petroli karibu na eneo la Dljirk Dahson mjini Mogadishu. Raia wawili wamethibitishwa kupoteza maisha na wengine watano kujeruhiwa. Hujuma hiyo imejiri karibu na makao makuu ya Wizara ya Mafuta na Uchimbaji Madini Somalia wakati wa msongamano mkubwa wa magari asubuhi. Hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na hujuma hiyo hadi sasa.

Lakini kundi la kigaidi la Al Shabab mara kwa mara hutekeleza mashambulio kama hayo ya kigaidi mjini Mogadishu kwa lengo la kuipindua serikali ya nchi hiyo inayotambuliwa kimataifa.

Magaidi wa Al Shabab wanaofungamana na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda walitimuliwa mjini Mogadishu mwaka 2011 lakini hutekeleza mashambulizi ya kuvizia mara kwa mara mjini humo.

Kuna askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika nchini Somalia, maarufu kama AMISOM lakini hawajaweza kurejesha amani ya kudumu nchini humo.

Wanajeshi wa AMISOM walioko Somalia ni kutoka Uganda, Kenya, Burundi, Somalia, Ethiopia, Djibouti na Sierra Leone. Nao maafisa wa polisi wa AMISOM ni kutoka Nigeria, Sierra Leone na Uganda.

AMISOM ina askari wapatao 21,000 nchini Somalia ambao wanalinda amani katika nchi hiyo inayosumbuliwa na vita vya ndani kwa robo karne sasa.