Bunge la Misri lajadili hoja ya kuondoa kikomo cha muhula wa rais
Bunge la Misri leo Jumanne limeanza kujadili hoja ya kuondoa kikomo cha muhula wa rais, hatua ambayo huenda ikamruhusu Rais Abdulfattah al-Sisi wa nchi hiyo agombee zaidi ya mihula miwili iliyoruhusiwa na katiba.
Mbunge Haitham el-Hariri amesema kikao cha leo kitajadili hoja hiyo ambayo iliwasilishwa Jumapili iliyopita.
Hoja hiyo imewasilishwa bungeni baada ya Mahakama ya Cairo kuidhinisha ombi lililowasilishwa kwake na 'wananchi kadhaa' waliotaka Spika wa Bunge aitishe kikao cha kufanyia marekebisho kipengee cha 140 cha katiba, ambacho kinasema rais anapaswa kugombea mihula miwili pekee ya miaka minne minne.
Aidha marekebisho hayo yanataka kuwasilishwa na kuainishwa majukumu ya makamu wa rais, sanjari na kuhuishwa Bunge la Seneti.
Kwa mujibu wa rasimu ya hoja hiyo iliyoonekana na shirika la habari la Reuters, Sisi anaweza kubakia madarakani hadi mwaka 2034.
Iwapo marekebisho hayo yatapasishwa na Bunge, wananchi wa Misri watapewa fursa ya kushiriki kura maoni ya ima kuyaunga mkono au kuyapinga marekebisho hayo ya katiba.
Hii ni katika hali ambayo, al-Sisi amekuwa akikosolewa kwa kuwakandamiza wapinzani na hasa viongozi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin tangu ashike hatamu za uongozi kupitia mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2013.