Hofu ya Amnesty International baada ya Misri kupewa uenyekiti wa AU
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeeleza wasi wasi wake baada ya Misri kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa kiduru wa Umoja wa Afrika kwa mwaka huu 2019, likisisitiza kuwa ukandamizaji wa haki za binadamu umefikia katika upeo wa juu kabisa katika kipindi cha utawala wa Rais wa sasa wa nchi hiyo, Abdul Fattah al Sisi.
Najia Bouns Direnaim, Mkurugenzi wa Amnesty International katika eneo la Kaskazini mwa Afrika ametoa mwito kwa wananchama wa AU kuhakikisha kuwa Misri haitumii uenyekiti huo kukanyaga misingi na mikakati ya umoja huo ya kupambana na ukiukaji wa haki za binadamu.
Amesema kuikosoa serikali ya sasa ya Misri ni hatari kubwa kwa wanaharakati kuliko wakati wowote mwingine katika historia ya nchi hiyo.
Mkurugenzi wa Amnesty International katika eneo la Kaskazini mwa Afrika amebainisha kuwa, ukandamizaji huo unalenga zaidi wanachama wa harakati ya Ikhwanul Muslimin, waandishi habari, watetezi wa haki za binadamu, wanasheria na hata maafisa wa taasisi za michezo.
Ameongeza kuwa, kuna wafungwa elfu sitini wa kisiasa nchini Misri kutokana na ukandamizaji mkubwa unaoendelea tangu baada ya mapinduzi ya Julai 2013 yaliyoiondoa madarakani serikari halali ya Rais Muhammad Morsi, tofauti kabisa na madai yaliyotolewa na rais wa nchi hiyo kwamba, hakuna mfungwa wa kisiasa huko Misri.
Rais Abdul Fattah al Sisi wa Misri anatazamiwa kukabidhiwa rasmi uenyekiti wa Umoja wa Afrika katika kikao cha 32 cha AU kitakachofanyika kesho (Februari 10) katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.