Walinda amani watatu wafariki dunia katika ajali ya helikopta nchini Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51452-walinda_amani_watatu_wafariki_dunia_katika_ajali_ya_helikopta_nchini_sudan
Umoja wa Mataifa umesema kuwa, walinda usalama watatu wamepoteza maisha baada ya helikopta ya kijeshi ya Ethiopia kupata ajali ndani ya kituo cha askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa (UNISFA), kwenye eneo lenye mzozo la Abyei katika mpaka wa Sudan na Sudan Kusini.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Feb 10, 2019 04:06 UTC
  • Walinda amani watatu wafariki dunia katika ajali ya helikopta nchini Sudan

Umoja wa Mataifa umesema kuwa, walinda usalama watatu wamepoteza maisha baada ya helikopta ya kijeshi ya Ethiopia kupata ajali ndani ya kituo cha askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa (UNISFA), kwenye eneo lenye mzozo la Abyei katika mpaka wa Sudan na Sudan Kusini.

Taarifa kuhusu ajali hiyo iliyotokea jana imeongeza kwamba, helikopta hiyo ilikuwa imebeba wanajeshi 23 wa Ethiopia. Kumi kati yao wamejeruhiwa huku hali ya majeruhi watatu ikiwa mahututi. 

Kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani katika eneo la Abyei huko Sudan kimesema, chanzo cha ajali hiyo hakijajulikana. 

Mabaki ya helikopta iliyopata ajali

 

Ethiopia ndiyo nchi pekee yenye wanajeshi wake wa kulinda amani chini ya kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa (UNISFA), kwenye eneo hilo. Ina maafisa 4,500 wa kijeshi wanaolinda amani kwa jina la umoja huo katika jimbo hilo la Abyei lenye utajiri mkubwa wa mafuta ambalo Sudan na Sudan Kusini kila moja inadai kuwa eneo hilo ni lake. 

Mkuu wa kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa, Meja Jenerali  Gebre Adhana Woldezgu amesema kuwa, uchunguzi bado unaendelea. Amesema, wamesikitishwa sana na ajali hiyo na wanatuma salamu za rambirambi kwa familia za wanajeshi waliopoteza maisha yao kwenye tukio hilo.  

Helikopta hiyo ilikuwa katika safari zake za kawaida na ilikuwa inatokea kwenye eneo la Kadugli kwa ajili ya kufanya safari zake za kawaida za kukagua eneo la Abyei.