Kadhaa wauawa katika makabiliano baina ya jeshi la Misri na magaidi, Sinai
Mapigano kati ya askari usalama wa Misri na watu waliokuwa na silaha katika mkoa wa Sinai Kaskazini yamesababisha askari kadhaa na wanagambao kuuawa.
Msemaji wa jeshi la Misri amesema, wanamgambo saba wameuawa katika makabiliano hayo ya leo Jumamosi.
Amesema operesheni ya kusafisha mabaki ya wanamgambo inaendelea kwa sasa, na kwamba baadhi ya magaidi waliotoroka baada ya kichapo wana majeraha mabaya ya risasi.
Ingawaje hajatoa maelezo kuhusu idadi ya askari waliouawa au kujeruhiwa katika mapigano hayo, lakini duru mbili za kiusalama zimeliambia shirika la habari la Reuters kuwa, wanajeshi 15 wa Misri wameuawa au kujeruhiwa katika makabiliano hayo.
Kundi la kigaidi linalojiita Wilaya ya Sinai ambalo ni tawi la kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh nchini Misri linaendesha hujuma katika mkoa huo na limeshauwa makumi ya watu katika operesheni zake dhidi ya raia na askari kikosi cha ulinzi cha Misri.
Mapigano kati ya askari usalama wa Misri na watu wenye silaha katika mkoa wa Sinai Kaskazini yalishika kasi mwaka 2014 baada ya Rais Abdul Fattah al Sisi kushika madaraka ya nchi hiyo.