Waalgeria wapinga Bouteflika kugombea tena kiti cha rais
Makundi mbalimbali ya wananchi wa Algeria wamefanya maandamano leo wakipinga uamuzi wa Rais wa sasa wa nchi hiyo, Abdelaziz Bouteflika kugombea kiti hicho kwa mara ya tano.
Waandamanaji hao wamemtaka Bouteflika abatilishe uamuzi wake wa kutaka kugombea tena kiti cha rais. Vilevile walikuwa wakipiga nara zinatoa wito wa kubadilishwa mwelekeo wa nchi hiyo na kubeba bendera za rangi nyeusi kama alama ya kutangaza upinzani wao dhidi ya hali ya kisiasa nchini Algeria.
Maandamano hayo ya wananchi wa Algeria yamefanyika baada ya muungano wa chama tawala kumtangaza Abdelaziz Bouteflika kuwa mgombea wake katika uchaguzi ujao wa rais.
Bouteflika mwenye umri wa miaka 82 anaiongoza Algeria kwa awamu nne mtawalia tangu mwaka 1999. Uchaguzi wa rais wa Algeria umepangwa kufanyika Aprili mwaka huu wa 2019.