Kagame: Hata kama Rwanda isingekuwepo, Burundi ingelikuwa na matatizo tu
Rais Paul Kagame wa Rwanda amevunja kimya chake na kuzungumzia uhasama wa miaka kadhaa sasa kati ya nchi yake na Burundi, huku akisisitiza kuwa mvutano huo sio mkubwa kiasi ambacho serikali ya Bujumbura inataka uonekane.
Amesema Burundi ingelikuwa inakabiliwa na changamoto na matatizo yanayaoikumba hivi sasa hata kama Rwanda isingelikuweko katika uso wa dunia.
Rais Kagame ameyasema hayo katika mahojiano na gazeti la East African na kufafanua kwa kuhoji kuwa, "Burundi imesema wazi kuwa Rwanda ndiyo tatizo lake, lakini je iwapo Rwanda isingekuwepo, Burundi isingelikuwa na matatizo?"
Burundi na Rwanda zimekuwa katika mzozo tangu kulipojiri jaribio la mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais Pierre Nkurunziza hapo tarehe 13 Mei 2015.
Mgogoro huo ulishtadi mwaka jana, baada ya Rwanda kuwatimua nchini humo mamia ya wakimbizi wa Burundi, kitendo ambacho baadhi ya wadadisi wa mambo walisema kuwa kilichochewa na mgogoro huo wa nchi mbili hizo jirani.
Hivi karibuni, msuluhishi wa mzozo wa Burundi, Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa alijiuzulu wadhifa wake huo akilalamika kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki imemtelekeza katika kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa nchini Burundi.