Afisa wa Misri: Utawala wa Israel unalenga kuigawa Afrika vipande vipande
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amesema utawala wa Kizayuni wa Israel hivi sasa unafuatilia njama ya kuzigawa vipande vipande nchi za Afrika.
Kwa mujibu wa ripoti ya tovuti ya elnashra Soad Shalaby Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri ametoa kauli hiyo alipohutubu katika kikao kilichokuwa kikijadili maudhui ya "Umoja wa Afrika, Fursa na Changamoto" mjini Cairo.
Shalaby amesema njama hiyo ya kuzigawa nchi za Afrika vipande vipande inatekelezwa kupitia kuzichezea shere na kuzilaghai nchi za ukanda wa Mto Nile kwa lengo la kuishinikiza Misri.
Shalaby ameongeza kuwa, kwa kuzingatia njama hizo, Misri inapaswa kuimarisha uhusiano wake na Ethiopia.
Itakumbukwa kuwa, kufuatia mgogoro wa Misri na Ethiopia kuhusu mradi wa bwawa la kuzalisha umeme al-Nahdha, mnamo mwezi Mei 2018, rais wa utawala wa Kizayuni wa Israel Reuven Rivlin alitembelea Ethiopia.
Mradi huo wa Ethiopia unaungwa mkono pia na Sudan ambapo nchi hizo mbili zinasema kuwa, kila nchi ina haki ya kutumia vizuri rasilimali zake kujiletea maendeleo.
Itakumbukwa kuwa, maji ya Mto Nile ndio mshipa wa uhai kwa Misri kwa karne nyingi na mara zote Cairo imekuwa ikiichukulia kwa hisia kali kila hatua ya kutumia maji ya Mto Nile ambayo inaweza kupunguza kiwango cha maji ya mto huo yanayofika nchini Misri.