Mamia ya wanachuo waandamana nchini Algeria dhidi ya Bouteflika
Mamia ya wanafunzi wa vyuo vikuu wa Algeria wamefanya maandamano katika barabara za mji mkuu wa nchi hiyo Algiers, kupinga mpango wa rais wa nchi hiyo Abdulaziz Bouteflika, kugombea tena urais kwa muhula wa tano.
Katika maandamano hayo ya jana Jumanne, wanachuo hao walikuwa wamebeba mabango yenye jumbe za kukashifu azma hiyo ya Rais Bouteflika mwenye umri wa miaka 81. Baadhi ya mabango hayo yalikuwa yameandikwa: "Kwaheri Bouteflika" na "Algeria inataka Mabaliko".
Duru za habari zinaarifu kuwa, maandamano kama hayo ya wanachuo wa mji mkuu Algiers yamefanyika katika vyuo vikuu vingine katika miji mikubwa ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Haya yanajiri siku chache baada ya askari usalama wa Algeria kuwatia mbaroni makumi ya watu katika maandamano ya wananchi wenye hasira yaliyofanyika kwenye mji mkuu wa nchi hiyo Algiers, kupinga azma hiyo ya rais wa nchi hiyo ambaye ni mgonjwa.
Wanaharakati nchini Algeria walikuwa wametumia mitandao ya kijamii kutoa mwito wa kufanyika maandamano ya upinzani ya nchi nzima baada ya Sala ya Ijumaa iliyopita, dhidi ya Rais Bouteflika.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 81, anayetembea kwa kutumia kiti cha magurudumu na ambaye amekuwa akionekana hadharani kwa nadra tangu alipopatwa na ugonjwa wa kiharusi mwaka 2013, alitangaza tarehe 10 Februari kwamba, atagombea urais kwa mara ya tano, katika uchaguzi unaotazamiwa kufanyika mwezi Aprili mwaka huu.