Watu 6 wauawa katika hujuma ya kigaidi Mogadishu, Somalia
Watu wasiopungua sita wameuawa katika shambulizi la hujuma ya kigaidi kwenye mtaa wenye pilika nyingi wa Maka Al-Mukarama katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Ofisa wa polisi Mohamed Ahmed amesema katika hujuma hiyo ya Alhamisi, gari moja lililokuwa na mabomu limelipuka katika kituo cha ukaguzi cha mtaa huo, na kusababisha vifo vya watu hao sita na wengine 20 kujeruhiwa.
Mashuhuda wamesema mlipuko huu ni mkubwa kutokea nchini Somalia mwaka huu, na umeharibu majengo kadhaa ikiwa ni pamoja na hoteli na migahawa. Kundi la kigaidi la al Shabab linalofungamana na mtandao wa al Qaeda limedai kuhusika na hujuma hiyo.
Kundi la magaidi wakufurishaji al Shabaab mara kwa mara hufanya mashambulizi ya kuripua mabomu huko Mogadishu na katika maeneo mengine ya Somalia dhidi ya serikali na sehemu nyingine. Aidha kundi hilo limekuwa likitekeleza mashambulizi nje ya Somalia.

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika walioko Somalia, maarufu kama Amisom, hawajaweza kurejesha uthabiti na usalama kamili nchini humo hasa katika mji mkuu Mogadishu.
Askari wa Amisom ambao sasa ni 21,000, wamekuweko nchini Somalia tokea mwaka 2007 na aghalabu ya askari wa Amisom ni kutoka Uganda, Kenya, Burundi, Somalia, Ethiopia na Djibouti.