Kushadidi ghasia na machafuko nchini Algeria
Maandamano ya wananchi wa Algeria dhidi ya uamuzi wa Rais wa sasa wa nchi hiyo, Abdelaziz Bouteflika wa kutaka kugombea tena kiti cha urais katika uchaguzi ujao yameitumbukiza nchi hiyo katika mgogoro mkubwa wa kisiasa na hadi sasa watu wasiopungua 10 wameuliwa katika mapigano kati ya waandamanaji na polisi huko Algiers mji mkuu wa nchi hiyo.
Maandamano hayo yalianza wiki kadhaa zilizopita baada ya Rais wa sasa wa Algeria, Abdelaziz Bouteflika kutangaza rasmi kuwa atagombea tena kiti cha urais kwa muhula wa tano mtawalia. Maandamano hayo yamepambana moto zaidi katika siku za karibuni. Bouteflika mwenye umri wa miaka 82 anaongoza Algeria kwa mihula minne tangu mwaka 1999 na sasa ametangaza kuwa atagombea tena kwa muhula wa tano. Kiongozi huyo ameahidi kuwa atafanya marekebisho katika muundo wa kisiasa, kiuchumi na kijamii wa nchi hiyo.
Japokuwa baadhi ya wanasiasa wa Algeria ukiwemo muungano wa chama tawala nchini humo wanamuunga mkono Bouteflika kuwa mgombea katika uchaguzi ujao wa rais na wanaamini kuwa hali ya usalama ya sasa ya Algeria matokeo ya jitihada zake na mpango wake wa mapatano ya kitaifa, lakini aghalabu ya wanasiasa na wanafikra nchini humo wanapinga ushiriki wa Bouteflika kwenye uchaguzi huo kiasi kwamba, siku kadhaa zilizopita mamia ya wanasiasa mashuhuri na wasomi wa Algeria walimwandika barua wakimtaka Rais Bouteflika asishiriki kwenye uchaguzi ujao wa rais. Wakati huo huo wapinzani wa serikai ya Algeria wanasema kuwa, Bouteflika amekuwa na utendaji dhaifu na wanapinga siasa za kiuchumi na kisiasa za kiongozi huyo.
Gazeti la al Watan limeyataja maandamano ya maelfu ya wananchi wa Algeria ya kupinga uamuzi wa Abdelaziz Bouteflika wa kutaka kugombea tena kiti hicho kwa mara ya tano mfululizo kuwa ni nukta muhimu ya kihistoria inayofunguliwa ukurasa mpya katika siasa za Algeria.
Wakati huo huo waandamanaji nchini Algeria wametangaza uungaji mkono wao kwa Rashid Nekkaz, mpinzani wa Abdelaziz Bouteflika katika uchaguzi ujao wa rais na wametaka kufanyika mageuzi nchini humo.
Wakati hu huo askari usalama wamekuwa wakitumia mabavu kuzuia maandamano ya wananchi bila ya mafanikio kutokana na wimbi kubwa la wananchi wanaojitokeza kwa wingi. Kwa msingi huo, Ahmad Ouyahia Waziri Mkuu wa Algeria ametishia kwamba, hatua kali zitachukuliwa dhidi ya maandamano yoyote yatakayofanyika kinyume cha sheria.
Algeria imetumbukia katika matatizo mengi na kwa muda sasa nchi hiyo inasumbuliwa na mgogoro wa kisiasa na kiuchumi. Kupungua mapato yanayotokana na mafuta ya petroli na utegemezi wa nchi hiyo kwa sekta hiyo kumezidisha matatizo ya kiuchumi, ukosefu wa ajira na kupanda gharama za maisha. Katika upande mwingine, baadhi ya marekebisho yaliyofanyika nchini humo, kuongezwa ushuru na kupungua huduma za bima yote hayo yamewafanya raia wengi wa Algeria wakabiliwe na hali ngumu ya kiuchumi. Katika uga wa kisiasa na kijamii pia kukosekana uhuru wa kijamii na kiraia na kuendelea hali ya hatari nchini humo kwa kipindi cha miongo miwili kumewapa sababu tosha wananchi wa Algeria kumiminika mitaani na kupinga suala la kugombea tena Bouteflika katika uchaguzi ujao wa rais.
Chama cha Vinara wa uhuru kimetoa taarifa kikitangaza kuwa, njia pekee ya kujikwamua nchi hiyo katika mgogoro wa sasa ni kujitoa Bouteflika katika kinyang'anyiro hicho na kwamba hatua hiyo inahesabiwa kuwa ni ya dharura kwa taifa la Algeria kwa ajili ya kulinda amani nchini humo.
Maandamano yanayoendelea sasa nchini Algeria ndiyo makubwa zaidi ya wananchi wa nchi hiyo baada ya malalamiko na ghasia kubwa zilizoshuhudiwa miaka kadhaa iliyopita katika nchi za kaskazini mwa Afrika. Kwa kuzingatia hayo yote inaonekana kuwa, katika siku zijazo Algeria itakabiliwa na hali ya mivutano itakayokuwa na taathira kubwa katika mustakbali wa kisiasa wa nchi hiyo.