Makumi ya maelfu ya Waalgeria waandamana kutaka rais Bouteflika ang'atuke madarakani
Makumi ya maelfu ya watu wameandamana katika miji mbalimbali nchini Algeria kutaka rais wa nchi hiyo Abdelaziz Bouteflika aondoke madarakani. Maandamano hayo ya jana Ijumaa ni makubwa zaidi kufanywa dhidi ya serikali tangu yale ya miaka minane nyuma wakati wa vuguvugu la Machipuo ya Kiarabu yaliyojulikana pia kama Mwamko wa Kiislamu.
Mashuhuda wameeleza kuwa, awali maandamano hayo yalikuwa ya amani, lakini baada ya idadi ya waandamanaji kuongezeka katika mji mkuu Algiers, fujo na makabiliano yalizuka kati ya askari polisi na waandamanaji hao karibu na Ikulu ya rais.
Afisa mmoja wa serikali amesema, mtu mmoja alifariki katika vurumai hizo, ambapo kwa mujibu wa vyombo vya serikali mtu huyo alikuwa mwanamme wa miaka 60 na kwamba kifo chake kilitokana na mshtuko wa moyo.
Televisheni ya taifa imeripoti kuwa waandamanaji kadhaa na polisi walijeruhiwa katika vurumai zilizotokea mjini Algiers. Mtandao wa habari wa TSA umenukuu taarifa rasmi zikieleza kuwa, watu 63 walijeruhiwa na wengine 45 walitiwa nguvuni katika maandamano hayo ya jana.
Umati mkubwa wa waandamanaji, wakiwemo vijana na wazee, walimiminika mabarabarani baada ya Sala ya Ijumaa hapo jana wakitoa nara za "Kwa heri Bouteflika!" na "Kwa amani, kwa amani," wengi wao wakiwa wamejitanda bendera ya Algeria na kubeba mabango na maberamu yenye maandishi mbalimbali.
Rais Abdelaziz Bouteflika, ambaye leo Jumamosi anatimiza umri wa miaka 82 amekuwa akiiongoza Algeria tangu mwaka 1999.
Kiongozi huyo anayetembea kwa kutumia kiti cha magurudumu na ambaye amekuwa akionekana hadharani kwa nadra tangu alipopatwa na ugonjwa wa kiharusi mwaka 2013, alitangaza tarehe 10 Februari kwamba, atagombea tena urais kwa mara ya tano, katika uchaguzi unaotazamiwa kufanyika mwezi Aprili.../