Chama cha Wafanyakazi kususia uchaguzi wa urais Algeria
Chama cha Wafanyakazi nchini Algeria kimetangaza kuwa hakitashiriki katika uchaguzi wa urais unaotazamiwa kufanyika Aprili 18 mwaka huu.
Hayo yalisemwa jana Jumamosi na Louisa Hanoune, Katibu Mkuu wa chama hicho, baada ya kufanyika mkutano usio wa kawaida wa Kamati Kuu ya Chama.
Siku ya Ijumaa Hanoune alidokeza kuwa chama hicho kinatathmini hali ya kisiasa nchini, na kingetangaza mwelekeo na msimamo wake jana Jumamosi.
Tayari vyama vikuu vya kisekula nchini humo vya Socialist Forces Front na Rally for Culture and Democracy vimetangaza kuwa vitasusia uchaguzi huo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, maandamano ya wananchi wa Algeria dhidi ya uamuzi wa Rais Abdulaziz Bouteflika wa kugombea tena kiti cha urais katika uchaguzi huo yameendelea kushuhudiwa nchini Algeria na kuitumbukiza nchi hiyo katika mgogoro mkubwa wa kisiasa.
Inaelezwa kuwa, hadi sasa watu wasiopungua 10 wameuawa katika mapigano kati ya waandamanaji na polisi huko Algiers mji mkuu wa nchi hiyo.
Rais Abdulaziz Bouteflika, aliyetimiza miaka 82 hapo jana na ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1999 kwa sasa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali ya Chuo Kikuu cha Geneva nchini Uswisi.