Rais wa Algeria asisitiza kugomeba urais huku maandamano dhidi yake yakishadidi
Hatimaye muhula wa mwisho wa kujiandikisha kisheria kugombea urais wa Algeria ulipowadia, Rais Abdelaziz Bouteflika, alijiandikisha rasmi kugombea tena katika uchaguzi huo. Katika barua yake kwa watu wa Algeria, ameahidi kuwa akichaguliwa atahakikisha kuna katiba mpya ambayo itapigiwa kura ya maoni na wananchi ili kuwepo mfumo mpya wa utawala nchini humo.
Aidha Bouteflika amesema ataanzisha sera za haraka za kuhakikisha utajiri wa nchi unasambazwa kwa usawa na kwamba ataondoa kila aina ya ukosefu wa uadilifu. Bouteflika anayekabiliwa na upinzani wa umma baada ya kuweko madarakani kwa muda wa miaka 20, amesema atagombea tena urais kwa mara ya tano katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi Aprili. Hii ni katika hali ambayo ana hali mbaya sana kiafya na daima yuko nje ya nchi kupata matibabu. Abdelghani Zaalane, mkuu wa timu yake ya kampeni ndiye aliyewasilisha karatasi zake za kugombea urais. Bouteflika amesema atawaandikia barua wananchi wa Algeria ambapo atawafahamisha kuhusu mpango wake kamili wa mustakabali.
Mgogoro wa kisiasa na maandamano ya wananchi yameshika kasi nchini Algeria katika wiki za hivi karibuni. Idadi kubwa ya Waalgeria hawataki Bouteflika agombee tena duru hii ya uchaguzi na wanasisitiza kuwa wanataka uchaguzi huru na wa haki. Vyombo vya habari na vyama vya kisiasa vinaamini kuwa, kutokana na uzee na maradhi yanayomsumbua, Bouteflika mwenye umri wamiaka 81, hana uwezo tena wa kuingoza nchi.

Hakim Boughar, mwandishi habari wa gazeti la Al Shaab anasema hivi: Mamilioni ya watu Algeria hawataki Bouteflika agombee tena urais na kwa hivyo yeye na wafuasi wake wanapaswa kufahamu ukweli huo. Ni wazi kuwa Bouteflika ni mgonjwa na urais unahitaji mtu mwenye afya na uwezo wa kiakili.
Aidha wananchi wengi wa Algeria wanakosoa utendaji kazi wa Bouteflika hasa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Kuongezeka matatizo ya kiuchumi, ukosefu wa ajira, kupungua huduma za kijamii na kuenea ufisadi ni kati ya matatizo ya sasa ya Algeria kwa matazamo wa waandamanaji. Ni kwa sababu hii ndio katika kipindi cha wiki za hivi karibuni serikali ya Algeria imetoa ahadi chungu nzima kujaribu kuwatuliza wananchi wenye hasira. Kati ya ahadi hizo ni kupunguza bei ya bidhaa za vyakula, kuimarisha demokrasia na kuondoa sheria ya hali ya hatari ambayo imekuwa nchini humo kwa muda wa miaka 19.
Ingawa waandamanaji walikuwa na matumaini kuwa Bouteflika hangegombea urais, lakini sasa baada ya kuwa ametangaza rasmi kuwa atagombea, maandamano yanatazamiwa kushika kasi. Mgogoro huo unaelekea kuwa mbaya zaidi baada ya vyama viwili vikubwa yaani Harakati ya Mujtamaa Salama, Hams, ambayo inahesabiwa kuwa chama kikubwa zaidi cha Kiislamu Algeria, na Chama cha Amal kutangaza kususia uchaguzi.
Msuguano wa kisaisa Algeria unatazamiwa kuwa mbaya huku waandamanaji wakisisitiza kudai matakwa yao ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.
Wakuu wa Algeria wameota wito kwa waandamanaji kusitisha maandamano yao lakini waandamanaji wamekataa na wanatahadharisha kuwa hali ya nchi hiyo yamkini ikawa kama ya Syria kutokana na uingiliaji wa madola ya kigeni.
Mustafa Hadam, mwanachama wa Harakati ya Al Mustakbla ya Algeria anasisitiza kuwa: "Kila wakati wananchi wa nchi za Kiarabu wanapodai haki zao, huwa kunaenezwa tetesi za kuwepo mikono ya ndani ya nchi na kigeni inayochochea hali ya mambo ili kuvuruga usalama." Anasema hadhani kuwa kuna chama chochote kinachotaka kutumia vibaya hali ya mambo nchini humo.
Katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa Aprili 18, Algeria itapitia kipindi kigumu ambacho kitaainisha mustakabali wa nchi hiyo na kuna uwezekano wa kushadidi machafuko ya kijamii na kisiasa nchini humo.