Rais Bouteflika azidi kubanwa; awaonya wafanya maandamano dhidi yake
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52033-rais_bouteflika_azidi_kubanwa_awaonya_wafanya_maandamano_dhidi_yake
Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria ametoa onyo lake la kwanza kwa maelfu ya raia wanaoandamana katika mitaa mbalimbali ya nchi hiyo wakitaka ahitimishe utawala wake wa miaka 20. Amesema kuwa ghasia na machafuko yatayumbisha nchi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 08, 2019 12:01 UTC
  • Rais Bouteflika azidi kubanwa;  awaonya wafanya maandamano dhidi yake

Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria ametoa onyo lake la kwanza kwa maelfu ya raia wanaoandamana katika mitaa mbalimbali ya nchi hiyo wakitaka ahitimishe utawala wake wa miaka 20. Amesema kuwa ghasia na machafuko yatayumbisha nchi.

Jana Alhamisi mamia ya mawakili waliandamana katika mitaa ya mji mkuu wa Algeria  wakipinga hatua ya Rais Bouteflika wa nchi hiyo ya kugombea tena kiti cha urais. Bouteflika mwenye miaka 82 na ambaye ni mgonjwa hajawahi kutoka hadharani na kuzungumza tangu apatwe na maradhi ya kiharusi mwaka 2013 na sasa inaelezwa kuwa Rais huyo amelazwa hospitalini mjini Geneva Uswisi.  

Mawakili wa Algeria wakiandamana dhidi ya Rais Bouteflika

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa na viongozi wa zamani wa Algeria wanasema kuwa kuna uwezekano majenerali wa jeshi la nchi hiyo wakaingilia kati iwapo maandamano yanayoendelea yatasababisha hali ya mchafukoge nchini humo.  Rais wa Algeria tayari amekabidhi fomu zake za ugombea wa kiti cha urais licha ya kusumbuliwa na maradhi. Jumuiya ya Taifa ya Mawakili ya Algeria imeitaka Tume ya Uchaguzi ya Nchi hiyo iakhirishe uchaguzi ujao wa rais na badala yake iunde serikali ya mpito.