Waasi wa Mai Mai wahujumu kambi ya kutibu Ebola nchini DRC
Waasi wa kundi la Mai Mai wamehujumu kambi ya kutibu wagonjwa wa Ebola huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kumuua afisa wa polisi kabla ya kutimuliwa na maafisa wa usalama.
Hujuma hiyo imefanyika leo Jumamosi katika kituo cha kutibu Ebola mjini Butembo na ni kituo hicho hicho kilichoshambuliwa wiki iliyopita na watu wasiojulikana na kupelekea shirika la misaada ya kitiba la Madaktari Wasio na Mipaka (Medecins Sans Frontieres) kusimamisha shughuli zake.
Wafanyakazi wa kutoa misaada wanawashuku sana wenyeji wa eneo hilo kuwa wanahusika katika uchochezi wa hujuma hizo.
Mashirika ya kutoa misaada yako mbioni kudhibiti mlipuko mkubwa zaidi wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambao hadi sasa umeua watu karibu 600 tokea Agosti mwaka jana. Jitihada za kudhibiti ugonjwa huo zimedororeshwa na makundi kadhaa ya waasi na wahalifu ambayo yanaendesha shughuli zao mashariki mwa DRC.
Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Daktari Tedros Adhanom Ghebreyesus alikuwa atembelee Butembo lakini haijulikani iwapo atafika eneo hilo. Meya wa Butembo, Sylvain Kanyamanda Mbusa amesema waasi hao wa Mai Mai wametimuliwa kwa mafanikio na kwamba kituo hicho sasa kiko chini ya ulinzi mkali.
Zaidi ya watu 800 nchini DRC wameathirika na Ebola katika mlipuko huu wa hivi karibuni zaidi ulioanza mwezi Agosti mwaka jana ambapo karibu 600 kati yao wamefariki dunia.
Hata hivyo kwenye maeneo kama Mangina, Beni, Komanda ugonjwa huo umedhibitiwa kwa kiasi kikubwa ambapo zaidi ya watu 250 wamepona na 80,0000 wamepatiwa chanjo dhidi ya Ebola.