Algeria yafunga vyuo vikuu, wanafunzi walaumiwa kuchochea maandamano
Serikali ya Algeria Jumamosi imeamuru vyuo vikuu vyote nchini humo vifungwe mapema kabla ya kuanza likizo ya msimu wa machipuo ili kujaribu kuzima kasi ya maandamano yanayoongozwa na wanachuo dhidi ya Rais Abdelaziz Bouteflika.
Amri ya Wizara ya Elimu ya Algeria imekuja siku moja baada ya makumi ya maelfu ya wananchi wenye hasira kuandamana katika mji mkuu, Algiers, wakitaka Bouteflika, ambaye amekua madakrani kwa muda wa miaka 20 aondoke uongozini.
Waalgeria ambao wamechoshwa na uongozi mbovu ambao umesababisha ukosefu wa ajira na ufisadi wamekuwa wakiandamana tokea Februari 22 wakimtaka Bouteflika, mwenye umri wa miaka 82, asitishe mpango wake wa kugombea urais kwa muhula wa tano mfululizo katika uchaguzi wa Aprili 18.
Maandamano ya Ijumaa yametajwa kuwa makubwa zaidi tokea mwaka 1991 wakati jeshi lilipobatilisha matokeo ya uchaguzi ambao chama cha Kiislamu cha FIS kilikuwa kimeshinda.
Bouteflika ametangaza nia ya kugombea urais katika hali ambayo amelazwa hospitalini mjini Geneva, Uswisi na hajawahi kuonekana hadharani tokea mwaka 2013 wakati alipopata kiharusi.
Wiki iliyopita, Jeshi la Algeria lilisema litadhamini usalama na halitaruhusu nchi hiyo irejee katika zama za umwagikaji damu. Akizungumza Jumanne, Mkuu wa Majeshi ya Algeria, Luteni Jenerali Ahmed Gaid Salah, bila kutaja majina, alisema kuna wale ambao wanataka nchi hiyo irejee katika "miaka ya machungu", akiashiria vita vya ndani nchini humo katika muongo wa 90.