Mshindi wa Tuzo ya Nobel akosoa serikali ya umoja wa kitaifa DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52074-mshindi_wa_tuzo_ya_nobel_akosoa_serikali_ya_umoja_wa_kitaifa_drc
Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel ameitaja kama usaliti kwa wananchi, hatua ya Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kukubaliana na mtangulizi wake, Joseph Kabila kuunda serikali ya umoja wa kitaifa katika nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 10, 2019 10:17 UTC
  • Mshindi wa Tuzo ya Nobel akosoa serikali ya umoja wa kitaifa DRC

Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel ameitaja kama usaliti kwa wananchi, hatua ya Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kukubaliana na mtangulizi wake, Joseph Kabila kuunda serikali ya umoja wa kitaifa katika nchi hiyo.

Katika mahojiano na shirika la habari la AFP, Dakta Denis Mukwege raia wa DRC amemtaka Rais Tshisekedi kufutilia mbali makubaliano hayo na Kabila.

Akimhutubu Rais Kabila, Mukwege amesema, "Ingawaje tayari umeshasaini makubaliano ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa kati ya chama chako na cha Kabila, lakini hujachelewa sana kughairi msimamo huo. Jiepushe na kusaliti azma ya wananchi ya kushuhudia mabadiliko ya kweli."

Taarifa ya pamoja iliyotolewa na Rais Tshisekedi na Joseph Kabila siku chache zilizopita ilisema kuwa, licha ya muungano wa FCC wa Kabila kuwa na wingi mkubwa bungeni lakini katika kuidhinisha matakwa ya wapiga kura, pande mbili hizo zimefikia maamuzi ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa. 

Washindi wa Tuzo ya Kifahari ya Nobel 2018

Wawili hao walikutana siku moja kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini DRC mwezi Disemba mwaka jana, ushindi ambao haujawahi kutambuliwa na Kanisa Katoliki nchini humo, linalodai kuwa mgombea wa upinzani Martin Fayulu ndiye aliyeibuka mshindi.

Oktoba mwaka jana, Denis Mukwege, daktari bingwa wa upasuaji raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na mwanaharakati wa Iraq, Nadia Murad walitangazwa washindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa mwaka huo 2018.