Bouteflika alazimika kutengua azma yake ya kuwania urais Algeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52109-bouteflika_alazimika_kutengua_azma_yake_ya_kuwania_urais_algeria
Baada ya mashinikizo na maandamano ya karibu mwezi mmoja, hatimaye Rais Abdelaziz Bouteflka wa Algeria amefutilia mbali azma yake ya kugombea tena urais katika uchaguzi ujao nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 11, 2019 23:51 UTC
  • Bouteflika alazimika kutengua azma yake ya kuwania urais Algeria

Baada ya mashinikizo na maandamano ya karibu mwezi mmoja, hatimaye Rais Abdelaziz Bouteflka wa Algeria amefutilia mbali azma yake ya kugombea tena urais katika uchaguzi ujao nchini humo.

Bouteflika alitoa tangazo hilo jana jioni na kuongeza kuwa, uchaguzi huo uliotazamiwa kufanyika mwezi ujao wa Aprili utasogezwa mbele kidogo, kwa ajili ya kutoa fursa ya kufanyika Kongamano la Kitaifa kuhusu mustakabali wa kisiasa nchini humo.

Tangazo hilo la Bouteflika la kutogombea urais katika uchaguzi ujao nchini Algeria liliwaripua vijana ambao walimiminika barabarani usiku wa kuamkia leo kusherehekea kile walichokitaja kama 'ushindi wa maandamano yao'.

Kabla ya tangazo hilo, mamia ya mahakimu wa nchi hiyo walitoa taarifa na kueleza bayana kwamba, hawatosimamia uchaguzi wa rais wa Aprili 18 ikiwa Bouteflika ataamua kuwania tena kiti hicho kwa mara ya tano mfululizo, na kukaidi wito wa upinzani mkubwa wa wananchi wanaomtaka aachane na azma yake hiyo.

Mbali na nchini Algeria, maandamano ya kumshinikiza Rais Abdelaziz Bouteflika ambaye ameiongoza nchi hiyo kwa miaka 20 asigombee tena urais kwa muhula wa tano yamekuwa yakifanyika pia nje ya nchi hiyo.

Maandamano ya wananchi wa Algeria dhidi ya Bouteflika

Wapinzani wanasisitiza kuwa, kiongozi huyo hana uwezo tena wa kuendelea kuongoza nchi kutokana na afya yake kudhoofika na kwa sababu ya kile wanachokiita ufisadi sugu na kukosekana mageuzi ya kiuchumi ya kukabiliana na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira kinachopindukia asilimia 25 kwa vijana wenye umri chini ya miaka 30 nchini Algeria.

Rais Abdelaziz Bouteflika mwenye umri wa miaka 82 na ambaye anatembea kwa kutumia kiti cha magurudumu, amekuwa akionekana hadharani kwa nadra tangu alipopatwa na ugonjwa wa kiharusi mwaka 2013