Ugonjwa angamizi wa tauni waibuka mpaka wa Uganda na DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52120-ugonjwa_angamizi_wa_tauni_waibuka_mpaka_wa_uganda_na_drc
Ugonjwa angamizi wa tauni umeibuka katika mpaka wa Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo hadi sasa watu kadhaa wanaripotiwa kupoteza maisha.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Mar 12, 2019 13:01 UTC
  • Ugonjwa angamizi wa tauni waibuka mpaka wa Uganda na DRC

Ugonjwa angamizi wa tauni umeibuka katika mpaka wa Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo hadi sasa watu kadhaa wanaripotiwa kupoteza maisha.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa huo umegunduliwa na wafanyakazi wa afya wa serikali ya Uganda katika wilaya ya Zombo. WHO imewapongeza wafanyakazi wa sekta ya afya ya Uganda kwa uwezo wao wa kutambua kwa haraka mlipuko huo wa tauni ambao unaua iwapo hautambuliki mapema na mgonjwa kutibiwa kwa dawa maalumu.

Wizara ya Afya ya Uganda imesema kesi mbili za tauni zilithibitishwa wilayani Zombe Machi 5 ambapo mwanamke aliyekuwa na umri wa miaka mitano alifariki dunia na binamu yake mwenye umri wa miaka 23 pia ameripotiwa kuwa na dalili sawa.

Uchunguzi umebaini kuwa mwanamke aliyefariki dunia alikuwa akiishi katika kijiji cha Atungulei katika mkoa wa Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kwamba mwanae aliyekuwa na umri wa miaka 4 alifariki dunia siku kadhaa kabla. Baada ya jamaa zake kubaini kuwa alikuwa mgonjwa katika mazishi ya mwanae, walimpeleka Uganda kupata matibabu. 

Wafanyakazi wa sekta ya afya nchini Uganda

Watu 55, wakiwemo 11 wa sekta ya afya walioshiriki katika maziko ya mwanamke huyo wametambuliwa na wanachunguzwa iwapo wana ugonjwa huo hatari wa tauni. WHO inasema watu wengine watatu wamefariki dunia DRC wakiwa na dalili za watu wengine waliofariki kwa tauni.  

Ugonjwa wa tauni huripotiwa mara kwa mara Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Madagascar na Peru. Hayo yanajiri wakati ambao wakuu wa DRC wangali wanakabiliana na ugonjwa hatari wa Ebola katika mikoa ya Ituri na Kivu Kaskazini ambako umeua zaidi ya watu 600 tokea Agosti mwaka jana.

Tauni au kipukusa (kwa Kiingereza plague) ni ugonjwa unaoathiri watu wengi sana unaosababishwa na bakteria Yersinia pestis ya familia Enterobacteriaceae.