Waniger waandamana kupinga uwepo wa askari wa kigeni nchini kwao
(last modified Sun, 17 Mar 2019 07:03:20 GMT )
Mar 17, 2019 07:03 UTC
  • Waniger waandamana kupinga uwepo wa askari wa kigeni nchini kwao

Mamia ya raia wa Niger jana Jumamosi walifanya maandamano makubwa katika mji mkuu wa nchi hiyo Niamey wakipinga uwepo wa askari wa kigeni katika nchi yao.

Katika maandamano hayo waandamanaji vilevile walipiga nara za kupinga sheria ya ushuru inayopaswa kutekelezwa mwaka huu wa 2019 ambayo wanasema ni ileile iliyopingwa katika miaka iliyopita ambayo wanadai inakiuka haki zao za kijamii. Waandamanaji vilevile wameikosoa serikali ambayo inadai kupambana na fikra za kupindukia mipaka na wahamiaji haramu nchini Niger kwa kukaribisha nchini humo askari wa kigeni wakiwemo wa Ufaransa, Ujerumani, Italia na Marekani, ambao hawajasaidia chochote katika kulinda raia wa nchi hiyo dhidi ya mashambulio ya magaidi. Wametaka pia serikali iwaachilie huru mara moja wafungwa wawili mashuhuri wa kisiasa wa nchi hiyo.

Magaidi wa Boko Haram

Askari wa kigeni waliingia nchini Niger baada ya Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo kudai kwamba wanajeshi wa kawaida hawawezi kutumika kwa ajili ya kupambana na makundi ya kigaidi na hasa magaidi wa Boko Haram. Hivyo askari hao wa kigeni walipelekwa nchini humo kwa kisingizio cha kutoa mafunzo maalumu kwa vikosi vya kupambana na magaidi. Licha ya kuwepo askari hao katika ardhi ya Niger lakini raia wa nchi hiyo wameendelea kushambuliwa na magaidi wa Boko Haram na askari hao kutochukua hatua yoyote ya kuridhisha.

Tags