Ripoti: US imetumia $ bilioni 22 kuisaidia kijeshi Israel tangu Oktoba 7, kiwango halisi ni zaidi
(last modified Wed, 09 Oct 2024 02:27:27 GMT )
Oct 09, 2024 02:27 UTC

Marekani imetumia zaidi ya dola bilioni 22 kwa ajili ya misaada ya kijeshi inayoupatia utawala wa Kizayuni wa Israel na kufadhili uvamizi na mashambulio yaliyofanywa na utawala huo haramu katika eneo hili kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa na Taasisi ya Watson ya Chuo Kikuu cha Brown kwa ajili ya Masuala ya Kimataifa na Umma ambayo imebainisha kuwa, Marekani imeipa Israel dola bilioni 17.9 kwa sura ya msaada wa kijeshi tangu utawala huo wa Kizayuni ulipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Ghaza Oktoba 2023.
 
Kwa kuzingatia kubadilika kwa thamani ya sarafu ya dola kutokana na mfumuko wa bei, kiwango hicho ni cha juu zaidi kutolewa na Washington kwa Tel Aviv kupitia misaada ya kijeshi.
 
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, kiwango hicho cha msaada wa kijeshi kinapita kile kilichotolewa na Marekani kwa utawala wa Kizayuni wakati wa vita vya Waarabu na Israel vya 1973.

Kwa mujibu wa tovuti ya Middle East Eye, kiwango hicho cha fedha kilichotolewa na serikali ya Washington ni karibu mara nne ya kiwango ilichoipatua Israel katika miaka ya 1980 wakati wa vita ilivyoanzisha dhidi ya Chama cha Ukombozi wa Palestina PLO nchini Lebanon, ukaliaji wake wa mabavu wa ardhi ya nchi hiyo kwa muda wa miaka 15, na vita vyake vya 2006 dhidi ya harakati ya Hizbullah.

 
Kwa mujibu wa ripoti ya Taasisi ya Watson, msaada huo kwa utawala wa Kizayuni unajumuisha ufadhili wa kijeshi, uuzaji wa silaha na uhamishaji wa silaha kutoka kwenye maghala ya silaha ya Marekani.

Ripoti hiyo inaangazia na kuonyesha jinsi kiwango cha dola za walipakodi wa Marekani ilizopewa Israel kama sehemu ya msaada wa kijeshi kilivyoongezeka katika mwaka uliopita.

Hata hivyo, waandishi wa ripoti hiyo wametanabahisha kuwa kiwango hicho cha dola bilioni 22 sio kamili, wakitoa mfano wa kile walichokieleza kama "juhudi za utawala wa Marekani za kuficha idadi kamili ya misaada na aina ya mifumo inayotoa kupitia ujanja wa kiurasimu."

Ripoti hiyo aidha imesema, Marekani imetumia ziada ya dola bilioni 4.86 kufadhili operesheni za kuiunga mkono Israel katika eneo, ikiwa ni pamoja na operesheni za mashambulio yake dhidi ya Yemen tangu vilipoanza vita dhidi ya Ghaza.../

Tags