Maelfu ya watu wanahitaji kuokolewa Msumbiji baada ya kimbunga cha Idai
Habari kutoka nchini Msumbiji zinasema kuwa, watu zaidi ya 15,000 wanahitaji kuokolewa haraka na kupewa hifadhi kufuatia kimbunga cha Idai kilichotokea hivi karibuni nchini humo na kusababisha vifo vya mamia ya watu.
Maafisa wa serikali wanasema kuwa, watu wengi wamekwama juu ya mapaa ya majengo, na juu ya miti baada ya kupoteza makaazi yao na kwamba, wanahitajia misaada.
Mashirika ya misaada ya kibinadamu yanasema kuwa, mji wa Beira ambao umeharibiwa na kimbuga hicho kilichosababisha upepo mkali na mafuriko, huenda ukawa salama kwa siku mbili au tatu zijazo baada ya maji kuondolewa.
Hadi jana watu zaidi ya 500 walikuwa wamethibitishwa kupoteza maisha Zimbabwe, Malawi na Msumbiji kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na kimbuga cha Idai na kuwaacha maelfu bila makazi na hivyo wanahitaji msaada wa dharura wa kibinadamu. Mamia wamejeruhiwa na wengine wengi hawajulikani waliko.
Aidha ripoti zinasema kuwa, zaidi ya watu milioni mbili na nusu wameathirika kutokana na upepo mkali na mvua zilizoletwa na kimbunga cha Idai katika eneo la Kusini mwa Afrika.
Kimbunga cha Idai kilipiga mji wa Beira katika jimbo la Sofala katikati mwa Msumbiji usiku wa Machi 14 na 15 ambapo kabla ya hapo kulishuhudiwa mvua kubwa na mafuriko katika nchi tatu ikiwemo Msumbiji, Zimbabwe na Malawi na kusababisha maelfu ya watu kufurushwa makwao, vifo na uharibifu wa mali.
Umoja wa Mataifa nao umetangaza kuwa, kimbunga cha Idai kimesababisha uharibifu mkubwa katika baadhi ya maeneo nchini Msumbiji, Malawi na Zimbabwe na kwamba, huenda hili ni janga baya zaidi la hali ya hewa kuwahi kushuhudiwa katika eneo la kusini mwa Afrika.