Makumi ya maelfu waandamana Algiers, mji mkuu wa Algeria
Makumi ya maelfu ya watu wameandamana katika mji mkuu wa Algeria, Algiers, kushinikiza kung'oka madarakani Rais Abdelaziz Bouteflika ambaye anatembelea kigari cha wagonjwa.
Televisheni ya al Mayadeen imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, makumi ya maelfu ya waandamanaji wamemiminika kwenye mitaa ya mji mkuu Algiers kulalamikia kuendelea kubakia madarakani Rais Bouteflika wakisisitiza kuwa Algeria inataka mabadiliko kwa njia za amani.
Waandamanaji hao walikuwa wamebeba picha za wakombozi na mashujaa wa Algeria walioendesha vita dhidi ya wakoloni huku wakiimba: "Hatutaki udikteta, tunataka uhuru."
Waandamanaji hao wamehimiza pia kufanyika mabadiliko ya kimsingi nchini Algeria bila ya uingiliaji wa madola ajinabi yasiyolipendelea kheri taifa hilo.
Wananchi wa Algeria aidha wamepinga njama zozote za kuchochea mizozo na mifarakano nchini mwao na kusisitiza kuwa Algeria yote ni moja na mgeni yeyote asiyelitaka kheri taifa hilo atakumbwa na upinzani mkali wa wananchi wote wa Algeria.
Wiki iliyopita, Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria aliakhirisha uchaguzi wa rais wa nchi hiyo baada ya kulegeza kamba na kusema hatogobea tena katika uchaguzi ujao wa rais.
Hata hivyo wananchi wana wasiwasi na hatua yake ya kuakhirisha uchaguzi huo wakisema huenda anatafuta muda zaidi wa kubakia madarakani.
Uchaguzi wa rais wa kabla ya wakati wake ulikuwa umepangwa kufanyika tarehe 18 mwezi ujao wa Aprili 2019 katika nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika.