Kikosi cha Umoja wa Mataifa Somalia, UNSOM, chaongezewa muda wa kuhudumu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52454-kikosi_cha_umoja_wa_mataifa_somalia_unsom_chaongezewa_muda_wa_kuhudumu
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la kuongeza muda wa kuwepo kwa Kikosi cha Kutoa Msaada cha Umoja wa Mataifa nchini Somalia UNSOM hadi tarehe 31, Machi mwaka 2020.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Mar 28, 2019 03:30 UTC
  • Kikosi cha Umoja wa Mataifa Somalia, UNSOM, chaongezewa muda wa kuhudumu

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la kuongeza muda wa kuwepo kwa Kikosi cha Kutoa Msaada cha Umoja wa Mataifa nchini Somalia UNSOM hadi tarehe 31, Machi mwaka 2020.

Kwa mujibu wa azimio hilo nambari 2461, UNSOM itaendelea kutoa uungaji mkono wa kimkakati na kutoa ushauri kwa serikali ya Somalia na Kikosi cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM kuhusu ujenzi wa amani na ujenzi wa mfumo wa serikali.

Azimio hilo limeitaka serikali ya Somalia na serikali za majimbo nchini humo kuharakisha utekelezwaji wa mabadiliko katika mfumo wa usalama ikiwa ni pamoja na kuibua muundo wa pamoja na usalama wa taifa.

Somalia ilitumbukia katika mapigano na machafuko ya ndani tangu ilipoondolewa madarakani serikali ya Mohamed Siad Barre mwanzoni mwa muongo wa 1990.  Mbali na harakati za kundi la kigaidi la al-Shabab kuwa tatizo kuu nchini Somalia, nchi hiyo inakabiliwa pia na ukame na baa la njaa.

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika, Somalia, AMISOM

Askari wa kulinda amani Somalia kutoka Umoja wa Afrika maarufu kama AMISOM  wanajumuisha wanajeshi 22,000 kutoka Kenya,  Burundi, Djibouti, Ethiopia na Uganda ambao walianza shughuli za kurejesha amani Somalia mwaka 2007. Askari wa AMISOM wamefanikiwa kuwatimua magaidi wakufurishaji wa Al Shabab kutoka maeneo mengi ya Somalia lakini magaidi hao wanaendelea kutekeleza mashambulizi ya kuvizia katika mji mkuu Mogadishu, na pia miji mingine katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.