Rais Tshisekedi wa DRC aruhusu maseneta kuanza kazi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52482-rais_tshisekedi_wa_drc_aruhusu_maseneta_kuanza_kazi
Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameondoa marufuku ya maseneta wapya kuanza kazi na hivyo kumaliza mgogoro uliokuwa umeibuka baina yake na rais aliyemtangulia Joseph Kabila, ambaye chama chake kilishinda viti vingi zaidi katika Bunge la Seneti.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Mar 29, 2019 11:21 UTC
  • Rais Tshisekedi wa DRC aruhusu maseneta kuanza kazi

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameondoa marufuku ya maseneta wapya kuanza kazi na hivyo kumaliza mgogoro uliokuwa umeibuka baina yake na rais aliyemtangulia Joseph Kabila, ambaye chama chake kilishinda viti vingi zaidi katika Bunge la Seneti.

Tshisekedi alikuwa amezuia maseneta hao wapya kuanza kazi mapema mwezi huu kutokana na madai kuwa, wajumbe katika mabunge ya mikoa, ambao huwachagua maseneta, walikuwa wamepewa hongo ya makumi ya maelfu ya dola kabla ya kupiga kura.

Hatua ya kuwazuia maseneta hao kuchukua nyadhifa zao ilionekana kama mbinu ya Tshisekedi, ambaye aliingia madarakani Januari, kuonyesha kuwa yuko na misimamo huru na hamtegemei Kabila. Chama cha Kabila Common Front for Congo (FCC) ndicho chenye viti vingi bungeni na rais huyo wa zamani ana ushawishi mkubwa pia katika vyombo vya usalama; na kutokana na kwamba alikuwa madarakani kwa muda wa miaka 18, nukta hizo zinatilia shaka uwezo wa Tshisekedi kuwa na utawala huru.

Rais wa zamani wa DRC Joseph Kabila

Katika taarifa, ofisi ya Tshisekedi imesema rais ameondoa marufuku ya maseneta kuanza kazi baada ya taarifa za awali za wachunguzi kubaini kuwa hakuna ushahidi wa ufisadi katika uchaguzi wa bunge la seneti. Chama cha Kabila cha FCC kilishinda viti 80 kati ya 100 katika Bunge la Seneti katika uchaguzi wa Machi 15 ikilinganishwa na viti vitatu tu vya chama cha UDPS cha Tshisekedi na waitifki wake.

Ushindi wa Tshisekedi katika uchaguzi wa rais mwezi Disemba nao pia ulikumbwa na madai ya wizi wa kura ambapo mgombea aliyeshika nafasi ya pili, Martin Fyulu alidai kuwa yeye ndiye aliyeshinda huku akimtuhumu Tshisekedi kuwa alifikia muafaka nyuma ya pazia na Kabila ili kubadilisha matokeo.