Maandamano makubwa yafanyika Algeria, Bouteflika akataa kung'atuka madarakani
Maandamano makubwa yamefanyika leo nchini Algeria huku wananchi wakiendelea kudai mabadiliko ya utawala wakati rais Abdelaziz Bouteflika amekataa kung'atuka madarakani hata baada ya kutengwa na jeshi.
Siku ya Jumanne, Mkuu wa Majeshi Luteni Jenerali Gaed Salah alilitaka baraza la kikatiba kutoa hukumu iwapo, Bouteflika, mwenye umri wa miaka 82 na ambaye ni mgonjwa sana, ana uwezo wa kuendelea kuwa rais au la.
Bouteflika, ameshindwa kuwatuliza waandamanaji wenye hasira hata baada ya kutangaza kuwa hatagombea urais kwa muhula wa tano baada ya kutawala kwa muda wa miaka 20.
Waandamanaji wanataka aondoke madarakani mara moja na kuwepo serikali ya mpito itakayoandaa uchaguzi huru na wa haki.
Wapinzani wanasisitiza kuwa, Bouteflika hana uwezo tena wa kuendelea kuongoza nchi kutokana na afya yake kudhoofika na kwa sababu ya kile wanachokiita ufisadi sugu na kukosekana mageuzi ya kiuchumi ya kukabiliana na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira kinachopindukia asilimia 25 kwa vijana wenye umri chini ya miaka 30 nchini Algeria.
Rais Abdelaziz Bouteflika mwenye umri wa miaka 82 na ambaye anatembea kwa kutumia kiti cha magurudumu, amekuwa akionekana hadharani kwa nadra tangu alipopatwa na ugonjwa wa kiharusi mwaka 2013.