Uchaguzi wa bunge ulioakhirishwa DRC wafanyika leo Jumapili
Uchaguzi wa Bunge ulioakhirishwa katika miji ya Butembo na Beni katika jimbo la Kivu Kaskazini pamoja na eneo la Yumbi katika mkoa wa Mai-Ndombe, Magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unafanyika leo Jumapili kama ilivyopangwa.
Wakazi wa maeneo hayo hawakushiriki uchaguzi wa Disemba mwaka jana kutokana na kile Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi nchini humo CENI ilichokitaja kama ukosefu wa usalama na mripuko wa ugonjwa hatari wa Ebola, ambao kufikia sasa umeshaua watu zaidi ya 650.
Usalama umeimarishwa katika maeneo hayo, huku vituo vya kupigia kura vikifunguliwa mapema leo. Viongozi wa maeneo hayo wametoa wito kwa wapiga kura kujitokeza kwa wingi kuwachagua wawakilishi wao.
Wabunge 15 wanatarajiwa kuchaguliwa katika uchaguzi huo uliocheleweshwa. Bunge la Kongo DR lina wabunge 500.
CENI iliakhirisha uchaguzi katika maeneo hayo matatu ya nchi hiyo ya Beni, Butembo na Yumbi kutokana na ugonjwa wa Ebola na mapigano ya kikabila yaliyoua mamia ya watu, hatua ambayo iliwanyima fursa wapiga kura zaidi ya milioni moja kushiriki uchaguzi huo.
Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, watu 535 waliuawa katika mapigano ya kikabila ya siku tatu katika mji wa Yumbi, siku chache kabla ya uchaguzi wa Disemba 30 mwaka jana.