Kuendelea mgogoro wa kisiasa nchini Algeria
Mgogoro wa kisiasa nchini Algeria ambao katika siku za hivi karibuni umeshadidi mno, sasa unaonekana kuchukua mkondo na wigo mpana zaidi.
Katika hali ambayo, Mkuu wa Majeshi Luteni Jenerali Ahmed Gaid Salah mara kadhaa ametaka kutekelezwa kifungu cha 102 cha Katiba na kumuondoa madarakani Rais Abdelaziz Bouteflik, jana Jumapili Bouteflika alitangaza kuunda baraza jipya la mawaziri. Baraza hilo jipya la mawaziri lina mawaziri 27.
Katika serikali hiyo mpya bado kuna nyuso za mawaziri waliotangulia. Kadhalika Waziri Mkuu Noureddine Bedoui amebakishwa katika wadhifa wake. Aidha katika serikali hiyo mpya, Bouteflika ameendelea kushikilia pia wadhifa wa Waziri wa Ulinzi. Hii ni mara ya pili kwa Rais Bouteflika kulifanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri katika kipindi cha miezi michache ya hivi karibuni.
Mara ya kwanza ilikuwa pale malalamiko ya wananchi nchini Algeria yaliposhika kasi na wapinzani kutaka Rais Bouteflika ang'atuke madarakani ambapo alimfuta kazi Waziri Mkuu na kuwabadilisha baadhi ya mawaziri na Wakuu wa Mikoa.
Mabadiliko makubwa ya kisiasa yanafanywa na Rais wa Algeria katika hali ambayo, katika majuma ya hivi karibuni mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo umeingia katika hatua mpya. Hali ilikuwa mbaya kiasi kwamba, wiki iliyopita, Mkuu wa Majeshi Luteni Jenerali Ahmed Gaed Salah kwa mara ya kwanza alilitaka Baraza la Katiba nchini Algeria litumie kifungu cha 102 cha Katiba na kutangaza kwamba, Rais Bouteflika hana tena uwezo wa kuongoza nchi.
Kwa mujibu wa kipengee hicho cha Katiba, endapo Rais wa nchi atakumbwa na maradhi sugu na hatari na akashindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, basi wajumbe wa Baraza la Katiba wataitisha kikao na baada ya kupitisha kwa kauli moja kwamba, Rais hana uwezo wa kuongoza nchi, uamuzi wao huo utawasilishwa Bungeni. Endapo Bunge litaidhinisha uamuzi huo kwa theluthi mbili ya kura, Spika wa Bunge atakaimu nafasi ya Urais kwa muda wa siku 45 na endapo afya ya Rais haitaboreka, Bunge litakuwa na jukumu la kumuuzulu.
Licha ya kuwa kuondoka madarakani Rais Abdelaziz Bouteflika yanahesabiwa kuwa moja ya matakwa makuu ya wananchi wa Algeria, lakini waandamanaji nchini humo wamekuwa wakitaka pia kuitishwa uchaguzi katika anga na mazingira huru na yenye misingi ya demokrasia.
Kimsingi ni kuwa, akthari ya wananchi wa Algeria wana hofu na wasiwasi mkubwa wa kuongezeka nguvu za jeshi nchini humo na kuwa na udhibiti wa madaraka.
Vyama vya upinzani nchini Algeria vimetangaza kuwa, wajumbe wa Baraza la Uongozi wa Mpito wanapaswa kuteuliwa kutoka miongoni mwa shakhsia wa kitaifa na ambao watakuwa na sifa za kugombea uchaguzi ulioko mbeleni. Aidha baraza hilo linapaswa kuwa na mamlaka ya Rais na katika kipindi cha miezi sita ijayo lichukue hatua ya kuchagua Baraza la Mawaziri stahiki, liunde Tume Huru ya Uchaguzi na kufanyia marekebisho sheria za uchaguzi.
Kwa sasa hali ya kisiasa nchini Algeria ingali tata. Baadhi ya tabiri zinaonyesha kuwa, katika kipindi cha siku chache zijazo, Rais Bouteflika na watu wake wa karibu watajiuzulu na kuunda baraza jipya la mawaziri katika fremu ya serikali ya mpito. Hata hivyo baadhi wanaamini kuwa, mabadiliko ambayo yanaweza kufanyika katika serikali ya Algeria kimsingi ni mabadiliko ya Bouteflika kumkabidhi madaraka mtu mwingine, hatua ambayo haitoi majibu ya kweli kwa matakwa ya kimsingi ya wananchi kuhusiana na demokrasia na kuweko mageuzi ya kimsingi ya kisiasa na kijamii katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Pierre Vermeren, mwanahistoria mtajika wa Kifaransa yeye sambamba na kuashiria kwamba, Algeria inahitajia mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii amesema: Kuweka kando mabaki ya viongozi wa kipindii cha kupigania uhuru ambapo Abdelaziz Bouteflika ni mmoja wao, kutekeleza siasa stahiki ambazo zinatabikiana na matakwa ya wananchi na kadhalika kuhitimisha utegemezi wa pato la mafuta sambamba na kuhuisha uzalishaji wa kitaifa ni miongoni mwa matakwa muhimu na ya kimsingi ya wananchi wa Algeria. Katika mazingira haya inaonekana kuwa, siku zijazo zitakuwa ngumu mno na zenye kuainisha hatima na majaaliwa ya wananchi wa Algeria.