Larijani: Marekani ni nembo ya ugaidi wa kimataifa kijeshi na kiuchumi
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa, serikali ya Marekani na majeshi ya nchi hiyo ni nembo ya ugaidi wa kimataifa, kijeshi na kiuchumi.
Jana Jumatatu, rais wa Marekani, Donald Trump alitangaza kuliweka Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH katika orodha ya Marekani ya makundi ya kigaidi.
Leo Jumanne, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu amesema katika kikao cha wazi cha bunge hilo kwamba jeshi la Sepah limekuwa na nafasi muhimu mno katika kupambana na ugaidi kwenye eneo hili. Ameongeza kuwa, kitendo cha Trump cha kudai kuwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kisilamu ni kundi la kigaidi kinaonesha ujinga na chuki kubwa mno ilizo nazo serikali ya Marekani kwa jeshi hilo la kimapinduzi.

Ameashiria pia nafasi muhimu wa askari wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu wakati wa vita vya miaka minane ambavyo Iran ililazimika kujihami baada ya kuvamiwa na utawala wa wakati huo wa Iraq na kuongeza kuwa, wakati huo jeshi la SEPAH lisisimama kiume na kishujaa kukabiliana na utawala wa Saddam ambao ulikuwa unaungwa mkono na madola yote duniani. Katika miaka ya hivi karibuni pia jeshi hilo limesimama imara kupambana na kuyashinda magenge ya kigaidi yaliyoundwa na kutiwa nguvu na Marekani kwa shabaha ya kuzusha vurugu kwenye eneo hili.
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran aidha amewakumbusha viongozi wa Marekani matamshi ya waziri mkuu wa zamani wa Pakistan, hayati Benazir Bhuto aliyesema kuwa, kiungo kikuu cha magenge ya kigaidi nchini Afghanistan ni Marekani, hivyo hivi sasa Marekani inapaswa kujibu ni kwa nini imeanzisha na kuunga mkono magenge hatari ya kigaidi.