Viongozi wa kisiasa wa Kongo watolewa wito wa kushiriki mazungumzo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i5275-viongozi_wa_kisiasa_wa_kongo_watolewa_wito_wa_kushiriki_mazungumzo
Mkuu wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amewatolea wito viongozi wa kisiasa wa nchi hiyo kushiriki mazungumzo ya kitaifa ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 17, 2016 10:50 UTC
  • Maman Sidikou
    Maman Sidikou

Mkuu wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amewatolea wito viongozi wa kisiasa wa nchi hiyo kushiriki mazungumzo ya kitaifa ya nchi hiyo.

Maman Sidikou, Mkuu wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Kongo (MONUSCO) amewataka viongozi wa kisiasa nchini humo kushiriki kwenye mazungumzo ya kitaifa kufuatia Baraza la Usalama kupasisha azimio nambari 2277 tarehe 31 mwezi uliopita. Maman Sidikou amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa unamuunga mkono Edem Kodjo, Waziri Mkuu wa zamani wa Togo ambaye ameteuliwa na Umoja wa Afrika kuwa Msuluhishi katika mazungumzo ya kitaifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Hii ni katika hali ambayo mazungumzo ambayo yaliitishwa na Rais Joseph Kabila wa Kongo tangu mwaka jana kuhusiana na mchakato wa uchaguzi, lengo likiwa ni kuendesha uchaguzi katika mazingira ya amani, bado yameendelea kuzusha mgawanyiko wa kisiasa nchini humo. Baadhi ya wapinzani wa serikali wamepinga mazungumzo hayo na kusema kuwa mazungumzo hayo yataandaa mazingira tu ya kumbakisha madarakani Rais Kabila. Muhula wa urais wa Rais Joseph Kabila unamalizika mwezi Disemba mwaka huu.