Maandamano yanaendelea Algeria licha ya ahadi za kufanyika uchaguzi huru
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52756-maandamano_yanaendelea_algeria_licha_ya_ahadi_za_kufanyika_uchaguzi_huru
Polisi katika mji mkuu wa Algeria, Algiers wamewafyatulia mabomu ya kutoa machozi maelfu ya wanafunzi waliokuwa wanaandamana kumpinga Spika wa Bunge Abdelkader Bensalah anayekaimu nafasi ya Abdulaziz Bouteflika, rais wa Algeria aliyelazimishwa kujiuzulu na maandamano makubwa ya wananchi.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Apr 10, 2019 11:40 UTC
  • Maandamano yanaendelea Algeria licha ya ahadi za kufanyika uchaguzi huru

Polisi katika mji mkuu wa Algeria, Algiers wamewafyatulia mabomu ya kutoa machozi maelfu ya wanafunzi waliokuwa wanaandamana kumpinga Spika wa Bunge Abdelkader Bensalah anayekaimu nafasi ya Abdulaziz Bouteflika, rais wa Algeria aliyelazimishwa kujiuzulu na maandamano makubwa ya wananchi.

Kwa upande wake, kaimu huyo wa rais wa Algeria ameahidi kufanyika uchaguzi huru na wa haki katika kipindi cha siku 90 zijazo. Akihutubia taifa kwa njia ya televisheni, Abdelkader Bensalah (76) alisema jana kuwa, kutaundwa tume huru ya itakayosimamia uchaguzi huo. Jana Jumanne pia, bunge la Algeria lilimuidhinisha rasmi spika huyo wa bunge kushika nafasi ya Abdulaziz Bouteflika.

Baada ya kuwa kaimu wa rais, sasa mamlaka ya spika wa bunge la Algeria yamepunguzwa na kazi yake kubwa kwa sasa hivi ni kuandaa uchaguzi wa rais katika kipindi cha siku 90 zijazo.

Abdelkader Bensalah

 

Kwa mujibu wa Katiba ya Algeria, Kaimu Rais hana haki ya kuunda serikali mpya wala kufuta Bunge na wala kugombea urais katika uchaguzi anaoandaa. Anapolazimika kutangaza hali ya hatari, katiba inamlazisha kuomba ridhaa ya wabunge na maseneta wanaopaswa kuchukua uamuzi katika kikao maalumu cha Bunge.

Vile vile hakuna marekebisho yoyote yanayoweza kufanywa wakati wa kipindi cha mpito cha miezi mitatu.

Kaimu Rais hawezi pia kutoa msamaha kwa wafungwa au kuitisha kura ya maoni katika kipindi chote cha kukaimu nafasi ya urais huko Algeria.