Apr 13, 2019 01:17 UTC
  • Ebola yaendelea kuua DRC, WHO kuitangaza hatari ya kimataifa

Wataalamu wa afya wa Shirika la Afya Duniani WHO wanafanya tathmini kubaini iwapo mripuko wa sasa wa ugonjwa wa Ebola ambao umeua mamia ya watu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unapaswa kutangazwa kuwa hatari ya kimataifa au la.

Msemaji wa WHO, Tarik Jasarevic amesema wataalamu hao wanachunguza taathira hasi na hatari ya ugonjwa huo kusambaa kimataifa. Profesa Robert Steffen wa jopo la wataalamu wa afya wa UN anatazamiwa kutoa tangazo hilo.

Wakati huohuo, watu wanne zaidi wameripotiwa kupoteza maisha kutokana na mripuko wa Ebola huko Kongo DR. Vifo hivyo vipya viliripotiwa jana Ijumaa katika maeneo ya mashariki mwa nchi.

Siku chache zilizopita, Wizara ya Afya ya Kongo DR ilitangaza kuwa, katika muda wa wiki tatu zilizopita, ugonjwa wa Ebola umeua zaidi ya watu 100; na zaidi ya watu 700 wamefariki dunia tangu mwezi Agosti Mosi mwaka jana kutokana na ugonjwa huo hatari.

Mkazi wa DRC akipewa chanjo ya Ebola

Kwa mujibu wa takwimu za WHO, tangu homa ya Ebola iliporipuka nchini humo mwezi Agosti mwaka jana 2018 hadi sasa, idadi ya watu waliothibitishwa kuambukizwa au wanaoshukiwa kuambukizwa imefikia 1,206 , na 764 kati yao wamefariki dunia.

Shirika la Afya Duniani limetahadharisha kuwa, mripuko wa ugonjwa hatari wa Ebola unasambaa kwa kasi nchini Kongo DR, ikiwa ni miezi minane sasa tangu ulipoanza kugunduliwa tena kwa mara ya pili.

Tags