Mwenyekiti wa Baraza la Katiba Algeria ajiuzulu huku maandamano yakiendelea
Mwenyekiti wa Baraza la Katiba nchini Algeria amejiuzulu huku maandamano ya wananchi yakiendelea katika miji mbalimbali ya nchi hiyo.
Tayeb Belaiz, alitangaza jana Jumanne kwamba, amekabidhi barua yake ya kujiuzulu wadhifa wake kama Mwenyekiti wa Baraza la Katiba kwa Abdelkader Bensalah, Rais wa mpito wa nchi hiyo.
Kujiuzulu Tayeb Belaiz, Mwenyekiti wa Baraza la Katiba nchini Algeria kunajiri katika hali ambayo, wananchi wa nchi hiyo wanaendelea na maandamano yao na miongoni mwa wanaoshinikizwa wajiuzulu ni Abdelkader Bensalah, Rais wa mpito wa nchi hiyo.
Waandamanaji nchini Algeria wanataka mabadiliko ya kimsingi ambayo yataandaa uwanja na mazingira ya kufanyika uchaguzi wa kidemokrasia wakiamini kwamba, kuweko mabaki ya viongozi wa serikali iliyopita ya Abdelaziz Bouteflika ni kikwazo cha kufikia lengo hilo.
Rais wa muda wa Algeria, Abdelkader Bensalah alitangaza hivi karibuni kuwa, tarehe 4 Julai mwaka huu ndiyo siku ya kufanyika uchaguzi wa kumtafuta mrithi wa Abdelaziz Bouteflika, rais wa nchi hiyo aliyejiuzulu.
Itakumbukwa kuwa, kufuatia maandamano makubwa ya upinzani ya kupinga serikali yaliyofanyika kwa muda wa wiki sita mtawalia nchini Algeria, hatimaye tarehe Pili Aprili Abdelaziz Bouteflika alitangaza rasmi uamuzi wa kujiuzulu wadhifa wa Urais baada ya kuiongoza nchi hiyo kwa kipindi cha miongo miwili.