Wananchi wa Misri wapiga kura 'kurefusha uongozi wa Sisi'
(last modified Sat, 20 Apr 2019 13:11:08 GMT )
Apr 20, 2019 13:11 UTC
  • Wananchi wa Misri wapiga kura 'kurefusha uongozi wa Sisi'

Wananchi wa Misri hii leo wameelekea katika masanduku ya kupigia kura kushiriki kura ya maoni, yenye azma ya kuondoa kikomo cha muhula wa rais, hatua ambayo huenda ikamruhusu Rais Abdulfattah al-Sisi wa nchi hiyo kugombea zaidi ya mihula miwili inayoruhusiwa na katiba.

Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa tatu asubuhi kwa saa za nchi hiyo, ambapo Rais Sisi alipiga kura katika wilaya ya Heliopolis, viungani mwa mji mkuu Cairo.

Waziri Mkuu, Mustafa Madbouly amewaasa wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo la siku tatu.

Vyama vya upinzani navyo vimewataka wananchi kupiga kura ya hapana ili kuangusha mpango huo, vikisisitiza kuwa marekebisho hayo ya katiba yatavunja misingi ya uhuru, demokrasia na uwepo wa utawala wa kiraia.

Wakati huohuo, mashirika mawili ya kutetea haki za binadamu ya Human Rights Watch na Kamisheni ya Kimataifa ya Majaji ICJ yameitaka serikali ya Misri kufutilia mbali mpango huo wa kuifanyia marekebisho katiba.

Bunge la Misri

Zoezi hilo la kura ya maoni linalofanyika kati ya leo Aprili 20 na Aprili 22, limekuja siku chache baada ya Bunge la Misri kupasisha muswada unaoruhusu kukifanyia marekebisho kipengee cha 140 cha katiba, ambacho kinasema rais anapaswa kugombea mihula miwili pekee ya miaka minne minne.

Iwapo wananchi wa Misri watayaunga mkono marekebisho hayo ya katiba kwa wingi wa kura katika kura hiyo ya maoni, huenda Sisi akabakia madarakani hadi mwaka 2030.

 

Tags