Kiongozi wa upinzani DRC awataka wananchi wamng'oe madarakani Rais Tshisekedi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53165-kiongozi_wa_upinzani_drc_awataka_wananchi_wamng'oe_madarakani_rais_tshisekedi
Kinara wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amewataka wananchi kutumia sauti na uwezo wao kumuondoa madarakani Rais Felix Tshisekedi wa nchi hiyo.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Apr 29, 2019 02:56 UTC
  • Kiongozi wa upinzani DRC awataka wananchi wamng'oe madarakani Rais Tshisekedi

Kinara wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amewataka wananchi kutumia sauti na uwezo wao kumuondoa madarakani Rais Felix Tshisekedi wa nchi hiyo.

Martin Fayulu alitoa mwito huo  jana Jumapili na kufafanua kuwa, "Nyinyi wananchi mna uwezo mkubwa kuliko jeshi lolote lile duniani. Katika nchi za Sudan na Algeria, wananchi waliungana na kuwang'oa madarakani marais wao. Hapa pia sisi lazima tufuate mkondo huo dhidi ya (Joseph) Kabila na (Felix) Tshisekedi."

Fayulu amemtaja Tshisekedi kama mtu anayefedhehesha na ambaye aliwauza wananchi mkabala wa maslahi yake ya kibafsi.

Tume ya Uchaguzi ilimtangaza Tshisekedi mshindi wa uchaguzi wa rais uliopita, kwa kupata asilimia 38.57 ya kura zote zilizopigwa huku Fayulu akiwa wa pili kwa asilimia 34.8. Mgombea wa chama tawala Emmanuel Ramazani Shadary, aliambulia asilimia 23.8 na kuibuka wa tatu.

Rais Tshisekedi (kushoto) na mtangulizi wake Joseph Kabila

Hata hivyo, Fayulu alidai kuwa yeye ndiye aliyeshinda uchaguzi huo kwa kupata asilimia 61 ya kura zote.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, viongozi wa Jukwaa la Lamuka ambao waliungana kumuunga mkono Martin Fayulu kama mgombea kiti cha urais wa Kongo DR katika uchaguzi uliopita na kisha mgombea huyo kushindwa, walikutana Ubelgiji na kugeuza jukwaa hilo kuwa chama cha kisiasa kikiongozwa na Fayulu.