Uchaguzi; changamoto kubwa katika matukio ya Algeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53341-uchaguzi_changamoto_kubwa_katika_matukio_ya_algeria
Mgogoro wa kisiasa nchini Algeria unaendelea kushuhudiwa huku suala la kufanyika uchaguzi wa Rais limegeuka na kuwa changamoto kubwa kabisa nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 07, 2019 20:56 UTC
  • Uchaguzi; changamoto kubwa katika matukio ya Algeria

Mgogoro wa kisiasa nchini Algeria unaendelea kushuhudiwa huku suala la kufanyika uchaguzi wa Rais limegeuka na kuwa changamoto kubwa kabisa nchini humo.

Abdelkader Bensalah, Rais wa Muda wa Algeria sanjari na kusisitiza juu ya kutekeleza ahadi zake kuhusiana na kufanyika uchaguzi katika tarehe iliyopangwa ameyaita makundi yote ya kisiasa na kiraia katika meza ya mazungumzo ya kitaifa, inagawa makundi hayo ya kisiasa na jumuiya za kiraia zimekataa wito huo.

Uchaguzi wa Rais nchini Algeria umepangwa kufanyika tarehe 4 Julai mwaka huu. Rais wa muda wa Algeria anasema kuwa, kuna haja ya kuweko mazungumzo ya kisiasa baina ya makundi ya kiraia na kisiasa kwa ajili ya kujadili mazingira mwafaka kwa ajili ya kufanyika uchaguzi ujao. Bensalah anaamini kuwa, kuna haja ya kufanyika mazungumzo ili kujenga hali ya kuaminiana na wakati huo huo kuandaa mazingira mwafaka ya kufanyika uchaguzi ujao katika anga tulivu na nzuri.

Maandamano ya wananchi wa Algeria

Hata hivyo wapinzani wanasisitiza kuwa, kuna haja ya kuweko kipindi cha mpito cha muda mrefu ambacho kitaongozwa na watu wasio na mafungamano na kipindi cha utawala uliopita wa Abdelaziz Bouteflika. Wapinzani nchini Algeria wanaamini kwamba, wakati wa kufanyika uchaguzi wa haki na wa kidemokrasia nchini Algeria haujawadia kwani kuna mambo mengi ya kurekebishwa na kuna mianya mingi ya kuzibwa kabla ya kufanyika uchaguzi huo.

Wapinzani hao wametangaza kuwa, hawatashiriki katika mazungumzo ya kitaifa na kusisitiza kuwa, kufanyika mazungumzo kama hayo ni aina fulani ya kupoteza muda. Abdallah Djaballah, Kiongozi wa Chama cha Uadilifu na Ustawi amesema kuwa, wito wa Rais wa muda wa Algeria wa kufanyika mazungumzo ya kitaiafa ni njama dhidi ya wananchi wa nchi hiyo na kuongeza kuwa, kama ambavyo hapo awali tulikataa wito wake wa kufanyika mazungumzo, mara hii pia tunatangaza upinzani wetu dhidi ya mazungumzo hayo.

Wananchi wa Algeria wanasisitiza juu ya kuuzuliwa shakhsia waliokuwako katika kipindi cha uongozi wa Abdelaziz Bouteflika nakisha kuuundwe Baraza la Uongozi litakalosimamia na kuongoza kipindi cha mpito. Wananchi hao wanasema, Abdelkader Bensalah, Rais wa Muda wa Algeria na Waziri Mkuu Noureddine Badawi shakhsia wakuu katika kipindi cha utawala wa Bouteflika wanapaswa kuondoka madarakani.

Abdelkader Bensalah, Rais wa Muda wa Algeria

Shakhsia hao wawili wanatambuliwa kama wafuasi na watu watiifu kwa  Abdelaziz Bouteflika na ndio maana akthari yya wapinzani na vyama vya siasa nchini Algeria wana wasiwasi kwamba, uwepo wao na ushirikkiano na jeshi unaweza kukwamisha juhudi za kufikiwa lengo la maandamano na malalamiko ya wananchi ambalo ni kuweko mageuzi ya utawala na kufikia demokrasia ya kweli.

Licha ya kuwa, Abdelkader Bensalah baada tu ya kuteuliwa kushika wadhifa wa  Rais wa Muda alichukua hatua kama za kuviita vyama vya kisiasa katika meza ya mazungumzo kuhusiana na namna ya kufanyika uchaguzi huru na wa wazi, kupambana na ufisadi, kuwatia mbaroni wafanyabiashara na maafisa wa serikali iliyotangulia ili kutuliza hali ya mambo, lakini inaonekana bado hajafanikiwa kwani upinzani na maandamano ni mambo ambayo yangali yanaendelea kushuhudiwa nchini Algeria.

Kwa mtazamo wa wapinzani ni kuwa, uchaguzi unapaswa kufanyika katika kipindi ambacho kuna anga ya uthabiti na utulivu katika nchi hiyo, mafisadi wawe wameshughulikiwa kwa mujibu wa sheria na watu wa karibu na watiifu kwa Bouteflika wasiwepo uongozini.

Abdelaziz Bouteflika, Rais wa zamani wa Algeria

Licha ya matakwa hayo ya wananchi, lakini Waziri Mkuu na Mkuu wa Majeshi wanasisitiza juu ya kufanyika uchaguzi haraka iwezekanavyo na kufuatiwa na hatua ya ukabidhianaji madaraka. Ahmed Gaid Salah, Mkuu wa Majeshi ya Algeria anasisitiza kwamba, uchaguzi wa Rais uliopangwa kufanyika Julai 4 mwaka huu ndio njia bora kabisa ya kuiondoa nchi hiyo katika mgogoro wa sasa wa kisiasa. Msimamo wa kamanda huyo wa jeshi na kung'ang'ania kwake kufanyika uchaguzi huo kumezidi kulipua ghadhabu na hasira za wananchi wa Algeria.

Akthari ya wanaopinga kufanyika uchaguzi kama huu wa kimaonyesho katika mazingira ya sasa wanaamini kuwa, hatua hiyo itakuwa ni kutekeleza malengo ya mabaki ya utawala wa Bouteflika. Kwa mujibu wa orodha ya wagombea iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Algeria ya watu waliotangaza nia ya kugombea kiti cha Urais hakuna shakhsia mashuhuri wa nchi hiyo anayeonekana katika orodha hiyo. 

Waandamanaji nchini Algeria wanasisitiza juu ya kuendeleza maandamano yao hadi pale watakapofikia malengo yao makuu na hivyo kuundwa serikali iliyotokana na uchaguzi huru. Hapana shaka kuwa, hatua ya Serikali ya Muda ya Algeria ya kukubali matakwa ya wananchi itakuwa na nafasi muhimu katika mustakabali wa kisiasa wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.