Fayez al Sarraj azungumza na Kansela wa Ujerumani kuhusu mgogoro wa Libya
Rais wa serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya amezungumza na Kansela wa Ujerumaini kuhusiana na hasara zinazosababishwa na mashambulizi ya Jenerali Khalifa Haftar katika mji mkuu wa Libya, Tripoli.
Fayez al Sarraj ameonana na Kansela wa Ujerumaini, Angela Merkeli mjini Berlin na kumueleza kwa ufupi hasara za mjini Tripoli zinazoendelea kusababishwa na mashambulizi ya kijeshi ya Jenerali Khalifa Haftar, anayeongoza wapiganaji wanaojiita Jeshi la Taifa Libya.
Katika mazungumzo hayo, Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya amezitaka nchi za Ulaya kuchukua msimamo wa pamoja wa kupinga mashambulizi dhidi ya mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.

Hivi karibuni serikali hiyo ya umoja wa kitaifa ilitangaza kukatisha uhusiano wake wa kiusalama na Ufaransa baada ya Paris kuchukua msimamo wa kumuunga mkono Jenerali Khalifa Haftar.
Tarehe 4 Aprili mwaka huu, Jenerali Khalifa Haftar alitoa amri kwa wapiganaji wake ya kuanzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya mji mkuu wa Libya kwa uungaji mkono wa moja kwa moja wa Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Misri na Ufaransa.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya watu 430 wameshauawa na zaidi ya 2000 wengine wamejeruhiwa tangu yalipoanza mashambulizi hayo. Watu 55 elfu wengine wanakadiriwa kukimbia makazi yao kutokana na vita hivyo.