Mjumbe wa UN ataka kuimarishwa hadhi ya wanawake nchini Libya
Hanna Serwaa Tetteh, mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya ambaye pia ni mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNSMIL ametoa mwito wa kuinuliwa hadhi ya wanawake nchini Libya.
Katika sehemu moja ya mwito wake huo alioutoa jana Jumamosi kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Wanawake, Tetteh amesema: "UNSMIL inatoa mwito kwa wadau wote wanaohusika na masuala ya Libya kuchukua hatua madhubuti za kuendeleza hadhi ya wanawake na wasichana, kuhakikisha haki zao zinalindwa na kuwapa fursa sawa za kuchangia katika nyanja zote za uchumi na kuleta mabadiliko chanya."
Pia amehimiza kuungwa mkono na kuwezeshwa wanawake kupitia kukuza upatikanaji jumuishi wa nafasi za uongozi na uchukuaji wa maamuzi nchini Libya.
Sehemu nyingine ya taarifa yake imesema: "Wanawake nchini Libya, hasa wale wanaohusika katika nyanja za huduma za umma na maeneo ya kisiasa, wanaendelea kukumbwa na changamoto kubwa. Vikwazo vya kimfumo, ubaguzi na vurugu vinaendelea kuzuia ushiriki wao kamili na wa maana."
Tetteh amesisitiza kuwa UNSMIL itaendelea kupigania haki za wanawake wa Libya sambamba na kuunga mkono ushiriki wao wa maana na salama katika ngazi zote za jamii.
Jumamosi ya jana pia, Wizara ya Masuala ya Wanawake ya Libya ilitoa mwito wa kuimarishwa nafasi ya wanawake katika nafasi za kuchukua maamuzi, kulinda haki zao na kupitisha sheria zinazounga mkono hadhi ya wanawake na kuhifadhi utu wao.