Russia kutuma wataalamu wa kijeshi nchini Kongo DR
Serikali ya Russia imetangaza kuwa imeazimia kutuma wataalamu wake wa kijeshi huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa ajili ya kuimarisha uwepo wake wa kijeshi barani Afrika.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, lengo la Russia la kuamua kutuma wataalamu wake wa kijeshi huko Kongo DR ni kuandaaa mazingira ya kukamilishwa upelekaji wa zana za kijeshi ambazo nchi hiyo imenunua kutoka kwa Russia sambamba na kushughulikia ukarabati na usimamiaji wa vifaa hivyo.
Wiki iliyoipita serikali za Kinshasa na Moscow zilifikia makubaliano ya kutumwa wataalamu wa kijeshi wa Russia huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa ajili ya kazi za ukarabati na usimamiaji wa zana na vifaa vya kijeshi ambavyo Russia iliiuzia Kongo miaka mingi iliyopita.
Inasemekana kuwa, hatua hiyo imechukuliwa ili kufungua mlango wa ushawishi wa Russia katika bara zima la Afrika na pia kuanzia Bahari Nyekundu hadi katika Bahari ya Atlas.
Wataalamu wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa, juhudi za Russia za kujiimarisha kijeshi huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zinafanyika kwa malengo makubwa ya kiistratijia ya Moscow ya kutaka kuwa dola kubwa barani Afrika na Asia na kuanza vita vipya baridi ulimwenguni ili kurejesha hadhi ya Umoja wa Kisovieti kwa Russia.