Mwili wa Etienne Tshisekedi Kufika DRC miaka miwili baada ya kifo chake
Mwili wa aliyewahi kuwa waziri mkuu na kiongozi wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Etienne Tshisekedi, umeondoka nchini Ubelgiji na kuelekea nyumbani zaidi ya miaka miwili baada ya kifo chake.
Mwili huo ulikuwa uondoke Ubelgiji jana Jumatano lakini shughuli hiyo ikaakhirishwa dakika ya mwisho kutokana na sababu za kilojistiki.
Hayati Tshisekedi ambaye mwanae, Felix Tshisekedi aliapishwa mwaka huu kuwa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya uchaguzi, alifariki dunia February mwaka 2017 mjini Brussels, Ubelgiji.
Tangu Tshisekedi alipoaga dunia wakati wa utawala wa Joseph Kabila, familia ya Tshisekedi ilikuwa ikivutana na serikali wakati huo kuhusu mahali ambapo mwili wake ulipaswa kuzikwa hali iliyosababisha kucheleweshwa kurejeshwa mwili huo DRC Congo.
Mwili huo sasa unatazamiwa kuwasili mjini Kinshasa leo tayari kwa mazishi yaliyopangwa kufanyika mwishoni mwa juma hili. Kwa miongo kadhaa Etienne Tshisekedi alikuwa akifanya harakati za kisiasa kama kiongozi wa upinzani lakini hakuwahi kushika nafasi hiyo ya juu mpaka anafariki.
Kamati ya mazishi ya Tshisekedi imesema kwa uchache inahitaji dola milioni mbili za Kimarekani kwa ajili ya mazishi huku baadhi wakisema bajeti inayohitajika ni dola milioni sita.
Kamati hiyo imetetea bajeti yake hiyo kubwa kwa kusema kuwa Tshisekedi alikuwa na nafasi muhimu katika kupigania demokrasia DRC. Hata hivyo wapinzani wamelaani vikali bajeti hiyo ya mazishi katika kipindi hiki kigumu kwa uchumi wa DRC.