Uchaguzi wa Rais Algeria uliokuwa umepangwa kufanyika Julai 4 waakhirishwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53877-uchaguzi_wa_rais_algeria_uliokuwa_umepangwa_kufanyika_julai_4_waakhirishwa
Baraza la kikatiba nchini Algeria limetangaza kuakhirisha uchaguzi wa rais ambao ulikuwa umepangwa kufanyika Julai 4 na kusema sababu ya uamuzi huo ni ukosefu wa wagombea. Uamuzi huo utapelekea kuongezeka muda wa mpito wa kisiasa jambo ambalo yamkini likaibua hasira zaidi za waandamanaji.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 02, 2019 22:58 UTC
  • Uchaguzi wa Rais Algeria uliokuwa umepangwa kufanyika Julai 4 waakhirishwa

Baraza la kikatiba nchini Algeria limetangaza kuakhirisha uchaguzi wa rais ambao ulikuwa umepangwa kufanyika Julai 4 na kusema sababu ya uamuzi huo ni ukosefu wa wagombea. Uamuzi huo utapelekea kuongezeka muda wa mpito wa kisiasa jambo ambalo yamkini likaibua hasira zaidi za waandamanaji.

Kufuatia uamuzi huo, yamkini rais wa muda Abdelkader Bensalah akaongezewa muda wa kubakia madarakani hadi atakapochaguliwa rais mpya. Abdelazizi Bouteflika alilazimika kujiuzulu kama rais wa Algeria kufuatia maandamano makubwa ya wananchi miezi miwili iliyopita baada ya kutawala kwa muda wa miaka 20.

Katika taarifa kupitia televisheni ya taifa Baraza la Katiba la Algeria limesema watu wawili waliojitokeza kugomeba urais hawakuwa wametimiza masharti.

Maandamano Algeria

Maelfu ya wananchi wa Algeria Ijumaa waliendelea kuandamana katika mji mkuu wa nchi hiyo Algiers na katika miji mingine ya nchi hiyo wakitaka kukabidhiwa kwa amani madaraka nchini.

Algeria hivi sasa inashuhudia mabadiliko ya kimsingi katika muundo wa kisiasa wa nchi hiyo, mabadiliko ambayo ni natija ya maandamano mtawalia ambayo yamekuwa yakifanywa na Waalgeria tangu Februari 22 mwaka huu.

Itakumbukwa kuwa wananchi wa Algeria walikuwa wakilalamikia hatua ya rais wa zamani wa nchi hiyo ya kugombea kwa muhula wa tano mtawalia. Maandamano yalishtadi nchini humo kupinga hatua hiyo na hatimaye Bouteflika akalazimika kujiuzulu kiti cha urais.